Yanga Vilio Tupu Mtaani....Hivi Ndivyo Al Hilal ya Ibenge ilivyoipelekea Moto Yanga

 

Yanga Vilio Tupu Mtaani....Hivi Ndivyo Al Hilal ya Ibenge ilivyoipelekea Moto Yanga

YANGA imeanza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifungwa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Al Hilal kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Swali kubwa lililoibuka baada ya matokeo hayo ni, tatizo nini?

Mabao ya Adama Coulibaly dakika ya 63 na Yasir Mozamil (dk 90) yaliitibulia Yanga ambayo haikuwa imeruhusu idadi hiyo ya mabao tangu irejee katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita baada ya takriban miaka 25.

Mabao hayo yalitokana na safu ya beki ya Yanga chini ya mabeki wa kati, Ibrahim Bacca na Dickson Job kutokuwa makini kuwazuia nyota wa Al Hilal.

Pia washambuliaji wa Yanga walishindwa kuwa na utulivu kwenye robo ya mwisho ya uwanja kutokana na namna timu hiyo imekuwa ikijenga mashambulizi.

Hata hivyo, msimu huu Yanga ilianza vizuri michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na hatua za awali hadi inafuzu makundi ilifunga mabao 17 bila ya nyavu zake kutikiswa.

Novemba 15 mwaka huu, Yanga ilifanya mabadiliko ya benchi la ufundi ikimwondoa Kocha Mkuu, Miguel Gamondi na msaidizi wake Moussa N’Daw, nafasi zao zikachukuliwa na Sead Ramovic na Mustapha Kodro.

Leo ndiyo kilikuwa kibarua cha kwanza kwa makocha hao ambao wameanza kwa kichapo cha aibu kilichoibua maswali mengi.

Katika dakika 45 za kwanza za mchezo huo wa Kundi A, Yanga ilionekana kuanza kwa kasi huku Al Hilal ikiwa taratibu lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda mambo yalikuwa yakibadilika.

Prince Dube ambaye leo alikabidhiwa mechi hiyo maalum ikipewa jina lake, alipata nafasi nyingi za kufunga lakini umakini mdogo ukaikosesha timu yake mabao.

Dakika hizo 45 za kwanza, Dube alikosa nafasi tatu za wazi ambao kama angekuwa makini basi angeifungia timu yake.

Bado kocha Ramovic atakuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha wachezaji wake wanashika falsafa zake akitaka kuona timu wanacheza soka la kasi lakini mbele kwenye umaliziaji.

Washambuliaji wa Yanga walishindwa kuwa na utulivu kwenye robo ya mwisho ya uwanja kutokana na namna timu hiyo imekuwa ikijenga mashambulizi.

Kukosa kwa nafasi hizo kumeendelea kuibua maswali ambapo Dube msimu huu amekuwa hana wakati mzuri kitakwimu ukiachana na mabao matatu aliyofunga hatua ya awali katika michuano hiyo, hana bao lingine.

Mbali na Dube kukosa nafasi hizo, lakini kukosekana kwa Khalid Aucho eneo la kiungo mkabaji imeonekana kuitesa zaidi Yanga na iliamua kumtumia Mudathir Yahya aliyesaidiana na Duke Abuya.

Viungo hao walionekana kushindwa kupandisha mashambulizi mbele na kuwaacha viungo wa Al Hilal kutawala eneo hilo licha ya kwamba Yanga ndiyo iliutawala mchezo kwa jumla kitakwimu za umiliki wa mpira.

Nguvu kubwa waliyokuwa nayo Al Hilal ilikuwa kutumia pembeni kufanya mashambulizi yake hasa upande wao wa kulia na Steven Ebuela alionekana kumsumbua beki wa kushoto wa Yanga, Nickson Kibabage.

Hata bao la kwanza lililofungwa na Coulibaly alitumia udhaifu wa upande huo wa Yanga, pia lile la pili lilipitia upande wa kulia wa Yanga.

Kwa ujumla, wachezaji wa Yanga katika mchezo wa leo walicheza kwa morali ya chini iliyowafanya kupoteza mchezo huo ikiwa ni mara ya pili mfululizo mbele ya Al Hilal.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Oktoba 16, 2022 katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa nchini Sudan na wenyeji Al Hilal kushinda 1-0. Kabala ya hapo, Oktoba 8, 2022 jijini Dar es Salaam, matokeo yalikuwa sare ya 1-1.

Ushindi huo unamfanya Kocha Florent Ibenge wa Hilal kuendelea kufurahia kukutana na Yanga kwani hajawahi kupoteza dhidi yao akishinda mara mbili nyumbani na ugenini na kutoa sare mara moja katika mechi tatu walizokutana.

Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge amesema: “Yanga ni timu kubwa, tulichokifanya ni kucheza kwa tahadhari, kipindi cha kwanza hakutuwa na mikakati ya ushindi, lakini kipindi cha pili ndiyo tulihitaji ushindi.

“Mpango huo ulikuwa ni kuhakikisha tunashambulia huku tukilinda lango letu kwa tahadhari kubwa baada ya kuona kipindi cha kwanza wapinzani wameshindwa kutufunga.”

Kocha Ramovic amesema: “Inaumiza, nimeanza namatokeo mabaya ya kipigo, kama timu kubwa tunarudi kujipanga na mechi zijazo, tunajua tuna mechi nyingi mbele, tutahamikisha tunafanya vizuri.

“Ukiangalia utimamu wa wachezaji upo chini kulinganisha na aina ya soka ninalotaka kucheza ni vitu tofauti hivyo kuna kazi ya kufanya kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri.

“Huu ni mwanzo, bado kuna mechi zingine za kucheza ambapo tuna wakati wa kusahihisha makosa ambayo tumeona leo yametokea ikiwemo kushinda kuzitumia vizuri nafasi tulizotengeneza.”

Licha ya Yanga kupoteza mchezo huo, inaweza kurudi na kufanya vizuri baada ya wapinzani wengine wa kundi lao, TP Mazembe na MC Alger kutoka 0-0 na kufanya msimamo kusomeka hivi; Al Hilal pointi 3, MC Alger (1), TP Mazembe (1) na Yanga (0).

Baada ya mchezo wa leo, Novemba 30 mwaka huu Yanga itakuwa ugenini kucheza na Namungo ukiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, kisha Desemba 6, itaenda Algeria kupambana na MC Alger iliyofungiwa na Caf mashabiki wake wasiingie uwanjani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad