Akizungumza na chombo cha habari cha BBC, Nondo alieleza kwa kina jinsi alivyokamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu na watu sita mara baada ya kuwasili katika Stendi Kuu ya Mabasi jijini Dar es Salaam, akitokea Kigoma alipokuwa kikazi.
Kwa mujibu wa Nondo, watekaji wake walikuwa wakimpa vitisho vya mara kwa mara, wakimtaka kunyamaza kuhusu kilichotokea.
"Walisema, 'Ukitoka hapa nenda moja kwa moja nyumbani kwako. Tunapajua vizuri, na usizungumze kokote juu ya kilichotokea.
Pia, tusikuone ukizungumza na vyombo vya habari. Ukifanya hivyo tutakuchukua na raundi hii tutakuua,’" alieleza Nondo kwa huzuni.
Nondo aliendelea kufafanua kuwa baada ya kutekwa, alipelekwa mahali pasipojulikana ambako alifanyiwa vitisho zaidi. Alidai kuwa tukio hilo lililenga kumtisha kutokana na nafasi yake kama kiongozi wa vijana wa upinzani.
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa tukio hilo lilimpa changamoto kubwa, lakini linaimarisha azma yake ya kupigania haki na demokrasia.
"Huu ni ujumbe kwa vijana wote wa upinzani, kwamba changamoto kama hizi hazipaswi kutukatisha tamaa," alisema Nondo huku akihimiza ujasiri na mshikamano.