Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo alitelekezwa maeneo ya fukwe za Coco, Kindondoni jijini Dar es Salaam na watu asiowafahamu.
“Baada ya kutelekezwa katika eneo hilo, Nondo alisimamisha bodaboda na kumwelekeza amfikishe katika ofisi za chama chake zilizopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam walifika muda wa saa tano usiku,” imeeleza taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kufika katika ofisi hizo, Nondo alionana na viongozi wake na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
“Baada ya kupatikana uchunguzi unaendelea, ili kuwapata wahusika wa tukio hili, ikiwa ni sambamba na kupata ukweli wa sababu au chanzo (motive) cha tukio hili, ili hatua nyingine za kisheria zichukuliwe,”imeeleza taarifa hiyo.
Tukio lilivyotokea
Nondo anadaiwa kukutwa na kadhia hiyo jana Jumapili, Desemba mosi, 2024 muda mfupi baada ya kushuka katika basi kituo cha mabasi cha Magufuli, jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Kigoma alikokuwa akishiriki shughuli za chama hasa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024
Baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, jana saa 6 mchana, Misime alitoa taarifa kwa umma akielezea tukio hilo lilivyokuwa kwa mujibu wa mashuhuda.
“Jeshi la Polisi lingependa kujulisha, Desemba mosi, 2024 saa 11.00 alfajiri katika eneo la stendi ya Magufuli Mbezi Louis, Dar es Salaam kuna mtu mmoja mwanamume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari lenye usajili wa namba T 249 CMV aina ya Land Cruiser rangi nyeupe.
"Ilielezwa na mashuhuda katika purukushani za ukamataji begi dogo lilidondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwemo vimetambuliwa ni vya Abdul Omary Nondo," ilieleza taarifa hiyo.