Chama cha ACT Wazalendo kimesema Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo Abdul Omar Nondo ametekwa na Watu wasiojulikana asubuhi hii leo December 01,2024 katika stendi ya Magufuli iliyopo Mbezi Luis Jijini Dar es salaam wakati akitokea Mkoani Kigoma alikokuwa sehemu ya Viongozi wa Kitaifa walioongoza kampeni kwenye Mikoa ya Magharibi mwa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi ACT Wazalendo, Mbarala Maharagande imesema Nondo aliwasili stendi ya Magufuli iliyopo eneo la Mbezi kwa usafiri wa basi la Saratoga lenye namba za usajili T 221 DKB na kwamba Mashuhuda wa tukio wanasema kuwa kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo iliyosababisha begi lake dogo la nguo na pingu iliyobebwa na mmoja wa Watekaji kudondoka.
“Katibu Mwenezi Mkoa wa Dar es salaam Monalisa Ndala na Afisa wa Harakati na Matukio Taifa, Wiston Mogha, waliofika mapema kituoni hapo walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Abdul Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye begi lililodondoka na notebook yake, Chama kinaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hili na kitatoa taarifa zaidi kwa umma, katika hatua ya sasa tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Cammillus Wambura kufuatilia haraka tukio hili na kuhakikisha Abdul Nondo anaachiwa huru mara moja”