Mabosi wa klabu ya Simba wanapiga hesabu kali ya kuimarisha kikosi kama mapendekezo ya kocha Fadlu David na sasa wamevuka mpaka hadi Uganda kufuata fundi wa mpira kiungo mshambuliaji, Allan Okello anayetumia mguu wa kushoto, ili kuja kuongeza nguvu.
.
Okello, mwenye umri wa miaka 24 amewahi kupita KCCA na Paradou zote za Uganda kwa sasa anakipiga Vipers iliyopo Ligi Kuu ya nchi hiyo, anayetajwa ni fundi wa mpira kwelikweli kwani analijua boli na inaelezwa kama atashuka Msimbazi na kuungana na wachezaji waliopo basi balaa litakuwa kubwa kwa wapinzani siku watakapokutana uwanjani iwe katika Ligi, Kombe la Shirikisho nchini au lile ya CAF, ikiwa Kundi A.
.
Hatua nzuri kwa Simba ni kwamba kama itampata fundi huyo atatumika moja kwa moja katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwani Vipers haikushiriki mashindano hayo msimu huu. Utata pekee wa Simba kumpata Okello ni uwepo wa Rais wa klabu hiyo, Lawrence Mulindwa ambaye amekuwa mtata kuachia mastaa wake muhimu wa kikosi hicho kuuzwa. Mulindwa ndiye aliyeweka ngumu kumuachia alive kuwa mshambuliaji wa timu hiyo Cesar Manzoki aliyekuwa anawindwa na Simba.
.