Ally Kamwe Atoa Mpya, Wakongo Walitupiga na Mawe na Makopo ila Hamkusema

Ally Kamwe Atoa Mpya, Wakongo Walitupiga na Mawe na Makopo ila Hamkusema


KLABU ya Yanga imelalamika kufanyiwa vurugu kubwa baada ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe, uliochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Mazembe, Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Akizungumza baada ya kurejea nchini kutoka DR Congo kwenye mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema mashabiki wa timu hiyo walipigwa na vitu mbalimbali kama chupa, mawe na viatu, wengine wakiporwa pesa zao, huku baadhi ‘wakitekwa’ na kulazimishwa kuimba.

“Tumefanyiwa fujo kubwa haijawahi kutokea, mimi nimesafiri na Yanga miaka miwili, huu ni wa tatu sasa, ila mechi hii tumefanyiwa fujo kubwa sana nawaambia ndugu zangu, jamaa wamefanya vitu vingi vya hovyo, kwanza kulikuwa na vitendo vya wazi vya kishirikina, lakini sijaona hata mchambuzi mmoja wa DR Congo aliyerekodi na kuposti.

“Sisi wote, mashabiki, viongozi wetu na wachezaji tumefanyiwa fujo sana, kuna wakati mashabiki wetu walichukuliwa wakawekwa mahala wakaambiwa wapige magoti waanze kuimba, yaani walikuwa na hasira sana baada ya ile sare,” alisema Kamwe.

Alisema kundi lingine la mashabiki liliwekwa kwenye jukwaa ambalo jua linapiga usoni, huku wakiwapiga marufuku wafanyabiashara kuwauzia maji.

“Mashabiki wengine waliwekwa eneo ambalo jua linapiga sana na wakapiga marufuku wasiuziwe hata maji ili kuwa tabu sana kwa sababu joto ambalo lipo Lubumbashi la sasa, hili la Dar es Salaam lina nafuu, lakini wachambuzi wao na watu wa habari wana uzalendo sana, hawajaandika, sijui ingetokea kwetu ingekuwaje. Nadhani wangerekodi na kuposti mitandaoni kuwa Klabu za Tanzania zimetesa watu.”

Alisema baada ya mechi kumalizika, mashabiki wa TP Mazembe wakiwa na hasira walitaka kwenda kuwapiga wachezaji wake, lakini kwa bahati mbaya sehemu ambayo walitaka kupita ndiyo wao walikuwa wamesimama.

“Mashabiki wa TP Mazembe walikuwa wanataka kwenda vyumbani kuwapiga wachezaji wao kutokana na sare waliyoipata, kwa bahati mbaya sana sisi tulikuwa tumekaa kwenye njia ambayo ndiyo walikuwa wanataka kupita, wakaanza kutupiga sisi kwanza, tumepigwa sana, tumepigwa na chupa, mawe, viatu na kila kitu, askari walichofanya ni kutuambia tukumbatiane ili hata kama tukipigwa silaha ziishie mgongoni na si usoni au sehemu nyingine ya mwili ambayo ingeweza kuwa ni ya hatari, mpaka baadaye sana tukaja kuokolewa na askari, lakini hali haikuwa nzuri kabisa, unaweza kuona kama ni utani, hatujafanyiwa fujo mashabiki wa Yanga ila ni Watanzania, mashabiki wamefika mpakani wakawekwa tena masaa sita kwa makusudi,”alisema.

Kamwe akabainisha kuwa kunapokuja suala la kizalendo waangalie ni namna gani ya kudili nalo kwani Congo kumefanyika mambo mazito lakini ipo kimya, hakuna hata mchambuzi mmoja aliyesema.

Naye kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic, alisema tayari ameanza kuona mwanga, kwani wakati anakuja kulikuwa na vitu vinne ambavyo vilikuwa anavifanyia kazi.

“Kwanza ilikuwa utimamu wa mwili wachezaji, kuingiza falsafa na staili ya kucheza, tatu tulikuwa na michezo migumu ya kimataifa na nne ni majeruhi, lakini mengi tumeyafanyia kazi na hali imeanza kuwa nzuri,” alisema.

Yanga ilitoka sare ugenini, ikisawazisha dakika za majeruhi kwa bao la Prince Dube, likiipa pointi moja na matumaini ya kufanya vema katika mechi tatu zilizobaki.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad