Kiongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, ametangaza kuhitimisha nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kanda hiyo, akitoa ujumbe wa kugusa moyo kwa viongozi na wanachama wa chama hicho katika mkutano uliofanyika Arusha.
Kupitia ujumbe aliotuma kusomwa na Katibu wa Kanda, Lema aliomba radhi kwa kutohudhuria mkutano huo, akieleza kuwa yuko na familia yake kwa mapumziko ya akili na amani ya moyo wake.
“Niliona ninapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya amani kubwa ya moyo wangu,” alisema.
Lema aliwataka viongozi wa Kanda ya Kaskazini kuwa makini katika uchaguzi wa viongozi wapya na kusisitiza nidhamu na heshima ndani ya chama.
“Lindeni sana nidhamu ya Kanda yetu, Mwenyekiti mwingine na Kiongozi yoyote wa ngazi yoyote asitukanwe wala kudhalilishwa, maana matusi na dhihaka zinaua sana morali ya kuwajibika,” alionya.
Akitafakari miaka zaidi ya ishirini aliyotumikia chama, Lema alisisitiza kuwa hajawahi kuzembea au kuigeuza harakati kuwa fursa ya hila dhidi ya yeyote.
Pia alieleza changamoto za kuwa kwenye siasa za upinzani, ikiwemo kupoteza marafiki, kupitia vipigo, kesi za mahakamani, na wakati mwingine upweke mkubwa.
“Ninaweza kula kiapo kuwa sijawahi hata siku moja kuwaza hila juu ya mmoja wenu, zaidi ya kujali ubora na mkakati wa kuimarisha kazi hii muhimu,” alisema.
Lema alihitimisha kwa kusisitiza kuwa uongozi si cheo bali utumishi, akiwataka viongozi wapya kuendelea kulinda heshima ya chama na kuimarisha umoja kwa maslahi ya nchi na chama.