Mwanachama maarufu wa Klabu ya Yanga SC, Haji Manara, ameomba radhi kwa mara nyingine kwa Jeshi la Magereza kufuatia sakata lililotokea wakati wa mechi ya Yanga SC dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa KMC.
Kupitia taarifa yake, Manara ameomba radhi kwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza, viongozi wa jeshi hilo, na askari wake wote kwa kile alichokielezea kama mazungumzo yaliyotokana na hisia za kishabiki.
Alikiri kwamba kauli zake za awali hazikuwa sahihi na alisisitiza kwamba hana neno bora zaidi ya "Samahani" kuelezea majuto yake.
"Heshima yangu kwa taasisi hii muhimu haiwezi kuwa na mbadala wa neno samahani," alisema Manara kwa unyenyekevu mkubwa, akionyesha heshima yake kwa Jeshi la Magereza na taasisi nyingine za dola nchini.
Manara pia alitumia fursa hiyo kusisitiza kwamba lengo lake halikuwa kudhalilisha au kukosea heshima kwa yeyote, bali hisia za kishabiki ndizo zilizopelekea hali hiyo.
Alitoa ombi la dhati la msamaha kwa wote waliokwazika kutokana na tukio hilo.