Wakili wa Msanii wa Marekani, Jay-Z anatarajia Msanii huyo ataondolewa katika kesi ya ubakaji wa Msichana wa miaka 13 inayomkabili yeye na Msanii mwenzake Diddy Combs baada ya maelezo ya Mshtaki wake kutofautiana na tukio hilo huku Baba yake akisema kuwa hakumbuki kama Binti yake alibakwa.
Wakili wa Jay-Z aitwaye Alex Spiro amesema kuwa Mteja wake hakutetereka baada ya kushtakiwa katika kesi hiyo ya madai wiki iliyopita ambapo anadaiwa kumbaka Msichana wa miaka 13 baada ya kumalizika kwa hafla ya utolewaji wa Tuzo za MTV VMA huko New York mwaka 2000.
Spiro amesema “kesi hii inahitaji kufutwa na jina la Carter (Jay-Z) linahitaji kufutwa kikamilifu, hana hatia kabisa na madai haya ni ya uongo lakini inasikitisha hakuna Mtu anataka kusikia mambo haya tunatarajia Carter kuondolewa katika siku zijazo.” amesema Spiro.
Maelezo ya Mshtaki anayedai kubakwa na Jay-Z na Diddy ambaye anaitwa Jane Doe hayaendani na matukio ya Tuzo za MTV na maeneo ambayo anasema alipelekwa kufanyiwa kitendo hicho hayaendani na muda aliotaja hata hivyo anadai kuwa Baba yake alikwenda kumchukua baada ya tukio hilo lakini Baba huyo amekana na kusema hakumbuki.
Kwa upande wa Wakili wa Mwanamke huyo Tony Buzbee amenukuliwa akisema “Mahakama zipo ili kutatua mizozo ya kweli, Mteja wetu anabakia kushikilia madai yake.” Uamuzi wa kesi hiyo unatarajia maamuzi ya mwisho ya Mahakama na Haki kutendeka kwa pande zote mbili.