Hii Ndio Maana ya Wimbo wa Kassongo Yeye



Bendi ya Soukous, Orchestra Super Mazembe.

Imekuwa kawaida vya zamani kurudi sasa na kupendwa zaidi. Hiyo yote ni kutokana na maendeleo ya teknolojia. Hilo linathibitika katika wimbo Kassongo (Kassongo Yeye) ambao kwa sasa umetegewa sikio upya na kupendwa na watu wengi kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakiutumia kama sehemu ya utani.

Fahamu kuwa wimbo huo uliimbwa na Orchestra Super Mazembe iliyokuwa bendi ya Soukous kutoka Kenya. Iliyoanzishwa awali mwaka 1967 huko Zaire kwa jina la 'Super Vox', kisha baadaye kundi hili lilihamia Nairobi nchini Kenya mwaka 1974 na kubadili jina lake kuwa Orchestra Super Mazembe.


Zipo nyimbo nyingi zilizoimbwa na kundi hilo lakini kati ya zilizopata umaarufu ni 'Shauri Yako', 'Bwana Nipe Pesa' na 'Samba'. Kwa upande wa 'Kassongo' licha ya kufanya vizuri miaka hiyo ya nyuma, umepata umaarufu zaidi siku za hivi karibuni baada ya mchungaji kutoka Uganda, Aloysius Bujingo wa kanisa la 'House of Prayer Ministries' lililopo Makerere kuuimba wimbo huo mbele ya waumini wake.

Hivyo kutokana na video za mchungaji huyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii imepelekea kuwavutia wengi hadi kuanza kuufanyia 'challange' kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo TikTok ambako umetumika na unatamba zaidi.

Licha ya wengi kuutumia wimbo huo kama kituko lakini waimbaji wake waliuimba makusudi kwa mistari hii ya Kilingala "Kassongo Yeye ee, mobali na ngai, Kassongo nga nawe oo, zonga libala ee" ikiwa na maana ya "Kassongo Yeye, mume wangu, Kassongo mimi na wewe, rudi kwenye ndoa".

Yaani wimbo huu ulimlenga mwanamke anayemuita mumewe, Kassongo, na kumwomba arudi nyumbani kuokoa ndoa yao. Ikumbukwe kuwa Kassongo ni kati ya nyimbo zilizopo kwenye albamu ya bendi hiyo iliyoachiwa January 4, 1980 na kupewa jina la 'Giants Of East Africa'.

Nyimbo nyingine zilizokuwa kwenye albamu hiyo iliyokuwa na nyimbo 11 ni Samba, Jiji, Gina, Mukala Musi,Mbanda Ya Mobange, Shauri Yako, Lukasi na nyinginezo

Licha ya hayo mwaka 2006, bendi ya Orchestra Super Mazembe ilibadili jina tena na kuwa Orchestra Bana Mazembe, baada ya wanachama wengi wa awali kufariki dunia.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad