Idadi vifo vilivyotokana na ajali iliyohusisha gari ndogo ya abiria aina ya Coaster iliyokuwa ikitokea mkoani Morogoro kuelekea Dar es Salaam na gari kubwa la mizigo lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro katika kijiji cha Bendera Mbili, tarafa ya Mikese Barabara Kuu ya Morogoro- Dar es Salaam imeongezeka kutoka watu 14 hadi kufikia 15.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amesema ongezeko hilo limetokana na majeruhi mmoja kati ya nane aliyelazwa katika hospitali hiyo kufariki dunia akiwa kwenye harakati za matibabu chini ya jopo la wataalamu.
Kwa upande wake Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Tanzania CP Awadh Juma Haji amefika eneo hilo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro, ambaye alikuwa akiyapita magari yaliyoko mbele yake (overtake) bila tahadhari.