Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kufuatilia na kubaini tukio la upotevu wa Daisle Simion Ulomi, aliyeripotiwa kutoweka mnamo Desemba 11, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya siku ya Jumatatu Desemba 16, 2024, ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Muliro J. Muliro, Ulomi aliondoka eneo lake akielekea Temeke kufuatilia biashara zake huku akitumia pikipiki yenye namba MC 415 DQC, ambayo alikuwa akiendesha mwenyewe. Hata hivyo, ufuatiliaji kwa kushirikiana na familia yake ulibaini kuwa Ulomi alipata ajali mbaya ya pikipiki maeneo ya Makuburi Ubungo External mchana wa siku hiyo (Desemba 11).
“Wasamaria wema walimsaidia kumpeleka kwenye Kituo cha Afya cha Makuburi External Ubungo akiwa hajitambui na hakuwa na kitambulisho chochote. Baadaye alipelekwa Mwananyamala hospitali na ikabainika tayari alikuwa amefariki na maiti yake kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mwananyamala kama mtu asiyefahamika akisubiri kutambuliwa na ndugu”, imeeleza taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa mwili wa marehemu ulikabidhiwa familia kwa taratibu za mazishi. Jeshi la Polisi limesema chunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea na taarifa zaidi itatolewa huku likiwataka wananchi kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali kama hizo.