Mathias pamoja na watu wengine watano walifikishwa mahakamani mnamo mwaka 2022, wakishitakiwa kwa njama za ulaghai na uhalifu ambao walikuwa wakimfanyia Pogba ambapo inadaiwa walimdai Pogba dola 14.3 milioni wakimtishia kuwa watafichua baadhi ya siri zake pia wakimtishia mara kwa mara.
Kundi hilo linatuhumiwa kufanya vurugu, utekaji nyara, na kumfunga Pogba ili kuwezesha ulaghai huo na wakati wa uchunguzi, Pogba alikiri kulipa dola 70,000 kwa kundi hilo akiwemo kaka yake. Mnamo Agosti 2022 Mathias aliposti video kwenye mitandao ya kijami, akidai kuwa angefichua taarifa za kushtua kuhusu kaka yake Paul.
Mathias alikamatwa muda mfupi baadaye na kufunguliwa kesi kwenye Mahakama ya Paris ambayo hukumu iliyotoka jana imempeleka gerezani kwa miaka mitatu, lakini wakili wake ameshasema kuwa watakata rufaa kuhusu hukumu hiyo kwa kuwa anaamini mteja wake hana hatia.
Paul Pogba (31) ambaye aliwahi kukiri kufikiria kustaafu soka kutokana na sakata hilo alibainisha kuwa alidanganywa na marafiki zake wa utotoni ambao walimshikilia mtutu wa bunduki mnamo 2022 na kumtaka awape €13m (£10.8m) ambapo aliwalipa €100,000 (£82,600).