Klabu ya Mamelodi Sundowns imemsimamisha kocha wa timu ya wanawake Jerry Tshabalala ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wasichana wa timu hiyo ambapo inadaiwa kocha huyo amekuwa akiingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya wasichana ikiwa wasichana wako uchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo wachezaji wa timu hiyo wamemlalamikia kocha huyo kutamka matamshi yasiyofaa ikiwemo kuwauliza ni mara ngapi huwa wananyoa sehemu zao za siri.
Vilevile kocha huyo anatuhumiwa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya timu hiyo na kugoma kutoka hata kama wachezaji hao wapo uchi wa ‘mnyama’ jambo ambalo linatafsirika kama unyanyasaji wa kijinsia.
Sundowns imempatia kocha huyo likizo maalumu kupisha uchunguzi huo huku ikiielekeza Mawakili kuchunguza madai ya mwenendo usiofaa wa kocha huyo na kutakiwa kuripoti mara moja kabla ya kuchukua hatua stahiki.
“Ikitokea uchunguzi utabaini ukweli unaothibitisha kwamba hatua zichukuliwe, bodi itachukua hatua zinazofaa mara moja. Mamelodi Sundowns itatoa taarifa kwa wakati kuhusu matokeo ya uchunguzi huo na hatua zitakazochukuliwa.” ——imesema taarifa ya klabu hiyo.