Mwanaharakati maarufu, Mange Kimambi, ameibua mjadala kuhusu uchaguzi wa ndani ya CHADEMA akieleza kwamba demokrasia ya kweli inapaswa kutumika kumpata mwenyekiti mpya wa chama hicho. Katika maoni yake, Mange ametaja sababu tano kuu za kumpongeza Tundu Lissu kama chaguo lake binafsi la uenyekiti huku akitoa changamoto kwa uongozi wa sasa unaoongozwa na Freeman Mbowe.
Mange amesisitiza kuwa, licha ya mchango mkubwa wa Mbowe katika historia ya CHADEMA, wakati wake umepita na chama kinahitaji mwelekeo mpya ili kurejesha ushawishi wake wa kisiasa.
Aliongeza kuwa makosa ya kihistoria kama kumkaribisha Edward Lowassa mwaka 2015, ambayo yaliathiri imani ya Watanzania kwa chama, ni sehemu ya sababu za kushuka kwa CHADEMA. Aidha, alihoji kuwa Lissu ameonyesha kuwa na maono mapana zaidi, jambo ambalo linatoa matumaini ya uongozi bora ndani ya chama.
Mange pia aligusia tofauti ya ushawishi wa kisiasa kati ya Mbowe na Lissu, akibainisha kuwa Lissu bado ana nguvu na ari ya kupambana kisiasa ikilinganishwa na Mbowe ambaye, kwa mujibu wa Mange, hana tena nguvu ya kuhamasisha wanachama.
Amehitimisha kwa kusema kuwa, demokrasia ni muhimu zaidi ya majina, lakini anapendekeza CHADEMA kupisha kizazi kipya cha viongozi wenye nguvu na mwelekeo wa kisasa ili kuimarisha demokrasia nchini.
Kwa tathimini ya kina, Mange ametoa rai kwa vyama vya siasa Tanzania kufuata mfano wa nchi nyingine kwa kuondoa viongozi waandamizi pindi wanaposhindwa kurudisha mwelekeo wa vyama vyao.