Mastaa Yanga Wafunguka Waliyopitia Kufungwa Mechi 3 Mfululizo

  

Mastaa Yanga Wafunguka Waliyopitia Kufungwa Mechi 3 Mfululizo

WACHEZAJI wa Yanga wamekiri kuwa walikuwa kwenye wakati mgumu baada ya kupoteza michezo mitatu mfululizo, kitu ambacho si cha kawaida kwa timu kubwa kama hiyo.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam juzi baada ya kutoka mkoani Lindi ilipokwenda kucheza dhidi ya Namungo na kushinda mabao 2-0 katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, kwa mara ya kwanza baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu na mmoja wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji hao walisema ushindi huo umewapa faraja na kuwarudisha kwenye matumaini ya kufanya vema kwenye michezo ijayo.

Nahodha Msaidizi, Dickson Job, alisema kulikuwa na presha ndani ya timu baada ya matokeo mabovu, lakini ushindi dhidi ya Namungo umeondoa kila kitu na sasa wanaangalia mbele, hasa katika mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya MC Alger nchini Algeria.

“Mchezo dhidi ya Namungo haukuwa rahisi kama watu walivyodhani, ulikuwa mgumu kwa sababu kuna presha ambayo ilianza kuingia kwenye timu baada ya kupoteza mechi zetu mbili za Ligi Kuu na ile ya kimataifa dhidi ya Al Hilal.

“Kikubwa kupoteza michezo ile maana yake tulikuwa nje ya malengo, lakini wachezaji tulitulia na kuangalia nini kinahitajika ili turejeshe makali yetu, kweli tumefanya hivyo na tumeshinda dhidi ya Namungo, ushindi ambao umetuweka vizuri sasa kuelekea kwenye mchezo wetu wa Jumamosi,” alisema Job, anayemudu kucheza beki wa pembeni na kati.

Yanga itacheza mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Juillet wa Tano jijini Algiers nchini Algeria, saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania.

Mchezaji mwingine, Duke Abuya, alisema ushindi walioupata unakwenda kwa mashabiki na kuwaomba msamaha baada ya kuwapa huzuni na kuwavunja nguvu, akiahidi kuwa hilo halitatokea tena la kupoteza michezo mitatu mfululizo.

“Tulikuwa kwenye wakati mgumu sana, kupata huu ushindi kimekuwa kitu cha maana sana, kimeturudisha wachezaji kwenye msitari.

“Nawaomba wachezaji wenzangu tuendelee na mwendelezo huu, tumewavunja nguvu na kuwahuzunisha mashabiki wetu, lakini sasa tuwafanye warudishe furaha yao walioizoea, niwaambie kuwa waendelee kutusapoti na hatutowaangusha tena,” alisema Abuya winga na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo ambaye tangu aje kocha Sead Ramovic amekuwa akimtumia kama kiungo mkabaji.

Yanga ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, uliochezwa Novemba 2, mwaka huu, katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kabla ya kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Tabora United Novemba 7, mwaka huu kwenye uwanja huo huo, na Jumanne iliyopita, ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad