Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ), imesema Mtumishi wake aitwae Amani Kamguna Simbayao amefariki dunia leo mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akitibiwa kutokana na kushambuliwa na Wananchi eneo la Tegeta kwa Ndevu, Dar es salaam jana akiwa kwenye majukumu yake ya kikazi baada ya kuhisiwa kuwa ni Mtekaji.
Taarifa ya TRA imesema Amani na Watumishi wenzake wawili wa TRA walishambuliwa wakati wakilifuatilia gari namba T229 DHZ aina ya BMW X6 ambalo imedaiwa liliingizwa Nchini kinyemela bila kulipa kodi stahiki za Serikali ambapo wakati wakiwa kwenye pilikapilika hizo walihisiwa kuwa ni Watekaji na kuanza kushambuliwa.
“Tunatarajia Wahusika wote watafikishwa kwenye Vyombo vya sheria, Mwenyenzi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema” —— imeeleza taarifa ya TRA