KLABU ya Simba imethibitisha kwamba, kila kitu kuhusu usajili wa Elie Mpanzu ndani ya kikosi hicho kimekamilika, hivyo ni rasmi sasa yupo tayari kuanza kuitumikia timu hiyo katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Jumamosi hii Desemba 21, 2024 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Septemba 30 mwaka huu, Simba ilitangaza kumsajili Mpanzu ikiwa ni wiki chache baada ya dirisha kubwa la usajili kufungwa Agosti 15, 2024 na iliezwa angeanza kutumika mara tu dirisha dogo lilipofunguliwa Desemba 15, 2024 lakini haikuwa hivyo kutokana na kutokamilisha baadhi ya taratibu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema Mpanzu ambaye amejiunga na timu hiyo kutoka AS Vita ya DR Congo ana asilimia kubwa ya kucheza dhidi ya Kagera Sugar.
Ally amebainisha hayo akiweka wazi kwamba kila kitu kuhusu usajili wake kwa maana ya vibali kimekamilika, kilichobaki ni benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids kuamua kumtumia kwani kiafya yupo vizuri.
“Elie Mpanzu ana asilimia 99.99 tarehe 21 akawa sehemu ya kikosi, mambo yake yote yameshakamilika na sasa yupo tayari kuitumikia Simba,” alisema Ally.
Katika msafara wa kikosi cha Simba uliosafiri leo Desemba 19, 2024 kwenda mkoani Kagera kwa ajili ya mchezo huo, Mpanzu alikuwa sehemu ya wachezaji wa timu hiyo jambo linalotoa majibu ya moja kwa moja yupo kwenye mipango ya benchi la ufundi.
Wakati Mpanzu akiingizwa kwenye usajili, ni wazi nyota mmoja wa kimataifa ameondolewa kikosini hapo ambapo awali Mwanaspoti lilikuhabarisha kwamba kipa Ayoub Lakred raia wa Morocco ndiye anakatwa.
Hatua hiyo inafuatiwa kwa sababu kabla ya ujio wa Mpanzu, Simba ilikuwa imekamilisha idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa wanaotakiwa kikanuni ambao ni Ayoub Lakred, Moussa Camara, Che Malone Fondoh, Chamou Karaboue, Valentine Nouma, Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua, Debora Mavambo, Steven Mukwala na Leonel Ateba.
Kuhusu nani anampisha Mpanzu, Ally amesema: “Tutatoa taarifa juu ya nani ameondolewa ili aingie Mpanzu, kuweni na subira.”
Mbali na Lakred, taarifa zinabainisha kwamba hata winga Mzambia, Joshua Mutale ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara anaweza kuachwa, lakini kuna mvutano ikielezwa kumetokea mgawanyiko kwa mabosi wa Simba juu ya uamuzi huo.
Mpanzu alichelewa kutua Msimbazi baada ya kupata dili la kwenda kufanya majaribio katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, mambo yalipokwama ndipo akasaini mkataba na Simba.