Msanii wa Nigeria, Burna Boy, ameibua gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuchapisha jumbe zenye mafumbo kwenye Instagram yake, ambazo wengi wameziona kama mashambulizi ya moja kwa moja kwa mwimbaji mwenzake, Davido. Hata hivyo, Burna Boy alifuta jumbe hizo muda mfupi baada ya kuzichapisha.
Kwenye InstaStory yake, Burna Boy aliandika:
- "Kama umewahi kudanganya kuwa ulinunua nyumba ya Sujimoto huko Banana wakati uliikodisha tu, fanya vyema mwaka 2025."
- "Kama umewahi kudanganya kuwa nyumba ya Elele ni yako, fanya vyema mwaka 2025."
- "Kama una saa ya ‘rainbow Daytona’ ya kubadilishwa na unawaambia watu ni halisi, tafadhali acha. Fanya vyema mwaka 2025."
- "Inapaswa kuwa kosa la jinai kusema uongo mwingi kama wanaume fulani."
Wadau wa burudani wamesema kuwa jumbe hizi zinahusiana na tetesi za muda mrefu kuhusu mvutano kati ya Burna Boy na Davido. Ingawa hakumtaja jina, ujumbe huu umeonekana kama mwendelezo wa ushindani kati ya wasanii hao wawili wa Afrobeat.
Hata hivyo, cha kushangaza ni kuwa Burna Boy aliamua kufuta jumbe zote muda mfupi baada ya Sujimoto kumjibu Burna Boy kuwa Davido alinunua nyumba kwao., jambo ambalo limezua maswali zaidi kwa mashabiki kuhusu nia yake halisi.
Mashabiki wa Davido na Burna Boy wamekuwa wakibishana mitandaoni, huku kila upande ukitetea msanii wao pendwa. Kwa sasa, haijulikani iwapo Davido atajibu mafumbo haya au ataamua kukaa kimya.
Muda utaamua iwapo mvutano huu utaendelea, lakini kwa sasa, ulimwengu wa Afrobeat unaendelea kushuhudia drama za mastaa wake.