Mtoto King John Mseke (9) ambaye ni Mtoto wa Msanii Staa wa Hiphop Tanzania Joh Makini ( @JohMakiniTZ ), amewasili katika Academy ya Club ya Manchester City iliyopo Jijini Manchester Nchini Uingereza kwa ajili ya mafunzo ya soka.
Joh Makini ameiambia @ayotv_ kuwa mwaliko huo kutoka Manchester City Football Academy ni nafasi kubwa na ya kipekee katika maisha ya King ambaye ndoto yake kubwa siku zote imekuwa ni kucheza mpira na kwamba haikuwa rahisi kufika Manchester City Academy kwani ni nafasi ambayo Joh amekuwa akiipambania kwa muda mrefu
“Ni stori ndefu sana, hivi ni vitu ambavyo tumekuwa tukitafuta wenyewe na kuvifanyia kazi kwa miaka kuhakikisha kipaji cha Mtoto kinaonekana, King alianza mafunzo serious akiwa na miaka minne au mitano baada ya kumuona ana kipaji ilibidi niivalie njuga sikutaka kuchukulia poa kabisa” - Joh Makini.
King ( @kingjmseke ) ambaye ni Mwanafunzi wa darasa la tano, aliondoka Tanzania kwenda Uingereza Ijumaa December 13 2024 ambako atakuwa kwenye mafunzo hayo ya Manchester City kwa muda wa wiki mbili “haya mafunzo unapata mwaliko kutokana na juhudi zako na uwezo wa Mtoto”.
“Wakishamaliza mafunzo wanaandaa ripoti jinsi walivyomuona Mtoto na pia wanakushauri vitu vya kufanyia kazi, unajua wale wako mbele sana wana vipimo vyao Mtoto anapimwa kila kitu yani wanaweza kukwambia mpaka shuti la huyu Mtoto uzito wake, mikimbio yake kitaalamu n.k, naamini hii safari yake itafungua milango mingi sana kwa huyu Mtoto” ——— Joh Makini.