Kocha wa Manchester City Josep 'Pep' Guardiaola (53), amesema kuwa huenda anastahili kufukuzwa kutokana na muendelezo wa matokeo mabovu wanayoyapata, baada ya jana kushuhudia timu yake ikipoteza mchezo wa nne mfululizo katika Ligi kuu ya Uingereza dhidi ya Liverpool pale Anfield.
Baada ya mchezo kuwisha Pep alisema: "Najivunia kushinda makombe sita ya Ligi Kuu ya Uingereza na sikutegemea mashabiki wa Liverpool kupiga kelele nifukuzwe, labda nastahili kufukuzwa kwa kweli".
Pep Guardiaola baada ya mchezo kumalizika alionekana akiwanyooshea vidole sita mashabiki wa Liverpool, ikiwa ni ishara ya mataji ya Ligi Kuu ya Uingereza ambayo ameshinda mpaka Sasa akiwa na Manchester City.
Aidha Pep katika mkutano na wanahabari aliongeza kuwa anaimani kila mtu katika timu yake atarejea katika hali yake ya kawaida, Kwa pamoja watapambana kuelekea mchezo wa Jumatano Desemba nne dhidi ya Nottingham Forest.
Manchester City imeshindwa kupata ushindi katika mechi saba mfululizo, ambapo mchezo wa mwisho kupata ushindi ilikuwa dhidi ya Southampton, Oktoba 26 mwaka huu.
Manchester City baada ya kipigo cha 2-0 hapo jana, wameshuka mpaka nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza, ikiwa na alama 23 baada ya michezo 13 tofauti ya alama 11 na vinara Liverpool.