Polisi Wamshakilia Dereva Aliyepiga Kelele Anatekwa Baada TRA Kutaka Kukagua Gari...



Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linamshikilia dereva aliyepiga kelele akidai anatekwa kwenye tukio lililosababisha wananchi kuwajeruhi watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Tukio hilo lilitokana na maofisa hao kulizuia gari alilokuwa anaendesha, “Kwa ajili ya ukaguzi wa magari yaliyoingia nchini bila kulipiwa kodi.”

Kwa mujibu wa TRA, gari hilo aina ya BMW x6 lenye namba T239 DHZ lilibainika kutokuwa ndani ya mfumo wa TRA na watumishi hao walipojaribu kulizuia, kuliibuka mzozo hadi dereva akipiga kelele kuomba msaada, akidai anatekwa.

Kukamatwa kwa dereva huyo kumedhibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipoulizwa na Mwananchi, leo Ijumaa, Desemba 6, 2024, kuwa yupo chini ya ulinzi pamoja na gari husika.

Maelezo ya TRA

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu utaratibu uliotumika kumkamata dereva huyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Richard Kayombo amejibu kwa njia ya maandishi: “Watumishi wa mamlaka hiyo hawakuwa kwenye ukamataji, bali walitaka kulikagua gari lile baada ya kubaini namba zake hazikuwa halali.”

“Hiyo T229 DHZ ni namba ya Nissan Civilian Bus sio BMW na (dereva) hakukamatwa, bali alisimamishwa kwa ajili ya ukaguzi na baada ya kugundulika kosa lake hatua zaidi zingefuata, ikiwepo kuwashirikisha polisi kwa sababu namba bandia na mambo mengine ikiwemo gari kutumika kwenye uhalifu au ukwepaji wa kodi,” ameandika.

Kayombo amesema watumishi waliojeruhiwa walikuwa maofisa wa forodha na walikuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Utawala wa Forodha wa Afrika Mashariki kuanzia kifungu 149 hadi 153.

Amesema maofisa hao wanapotekeleza majukumu yao hawahitaji kibali chochote cha mahakama.

Ilivyotokea

Mapema taarifa ya TRA imesema watumishi hao walijeruhiwa Desemba 5, 2024 wakiwa kwenye doria ya kudhibiti, ukamataji wa magendo na magari yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria.

Watumishi hao walilizuia gari hilo kwa mbele kwa gari aina ya Landcruiser huku wakimsihi dereva yule kuongozana nao, lakini alikataa akisema TRA hawafanyi kazi usiku, kwa mujibu wa mashuhuda.

Mashuhuda hao wamesema watumishi hao waliwapigia simu polisi kuomba msaada na wakati ubishani ukiendelea, dereva huyo naye alipaza sauti akiomba msaada kwa wananchi akidai anatekwa na watu ambao hawafahamu.

Shuhuda mmoja aliyezungumza na Mwananchi amesema baada ya kuona wananchi wanakimbilia eneo la tukio, alipiga simu polisi kuomba msaada kutuliza ghasia.

“Bada ya kuona hao watumishi wa TRA wamepiga simu polisi na hawajaja, niliwapigia na mimi na baada ya muda niliwafuata, kwa sababu tayari huyo dereva alishapiga kelele anatekwa watu waliendelea kukimbilia eneo la tukio wakiwa na mawe,” amesimulia shuhuda huyo.

Baada ya kufika kituoni na kutoa taarifa, shuhuda huyo amesema alipata mteja na kuondoka naye na hakurudi eneo la kujua kinachoendelea.

Hata hivyo, shuhuda mwingine ameeleza kuwa, baada ya maofisa wale kuzungukwa na watu ambao walikuwa wakiwarushia mawe wakiwaita watekaji, walianza kuondoa gari lao kuokoa maisha.

“Hawakufika mbali waligonga kitu kwa mbele na vioo vya gari lao vilipasuliwa na baadaye polisi walifika kutuliza ghasia zile,” amesema.

Kutokana na hayo, Kamanda Muliro amewatahadharisha wananchi kuepuka kujichukilia sheria mkononi kwani watajikuta matatani.

“Wananchi watajiingiza kwenye matatizo, waache kujichukuliwa sheria mkononi,” ameonya Muliro.

Mapema, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter naye ameandika: “Nimesikitishwa na tukio la kushambuliwa kwa watumishi watatu TRA na gari lao (STL 9923) walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kisheria ya kudhibiti magendo na magari yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria.”

Dk Mwigulu kupitia andiko lake hilo mtandaoni amewapa pole wote waliojeruhiwa na kuwaombea wapate nafuu haraka, akilaani tukio na kuahidi hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

“Aidha, TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu wa sheria. Tunatoa wito kwa wananchi wote kushirikiana na Serikali kuhakikisha sheria za kodi zinatekelezwa ipasavyo kwa maendeleo ya Taifa letu. Tukumbuke, "kodi zetu ndiyo maendeleo yetu," amendika Dk Mwigulu

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad