JESHI la Polisi limeingia mtaani kutoa elimu kwa umma ili kukomesha vitendo vinavyofanywa na matapeli wanaotuma ujumbe mfupi usemao ‘tuma kwa namba hii’.
Matukio ya utapeli wa namna hiyo yamekuwa yakiwasababishia wananchi hasara kutokana na kujikuta wakituma fedha kwa matapeli bila kujua kutokana na baadhi yao hujitambulisha wanatoka katika mitandao ya simu.
Kutokana hali hiyo, mara kadhaa Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata wanaodaiwa kujihusisha na utapeli huo na hata wengine kufikishwa mahakamani.
Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Beatrice Charles, akitoa elimu hiyo jana kwa wananchi maeneo ya Mikocheni mkoani Dar es Salaam, aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa polisi pale unapotokea uhalifu ili kufahamu namna ya kuwapata wanaojihusisha na utapeli mtandaoni.
Aliwataka wenye taasisi, kampuni kutunza vizuri taarifa za wafanyakazi wao, kwani wasipofanya hivyo kutoa mwanya kwa matapeli kuhakiki taarifa zao na kuwatapeli.
“Pia watumiaji wa simu wanapaswa kuhakiki taarifa za watu wanaowapigia simu na kusema ‘tuma pesa kwa namba hii’ au ‘nimetuma pesa kimakosa’” alisema Beatrice.
Alionya kitendo cha wananchi kushiriki katika masuala ya kihalifu akisisitiza kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Inspekta Msaidizi wa Jeshi la Polisi Waziri Makang’ila, alisema kosa la utapeli huingia kwenye jinai kwa kuwa linakiuka sheria za nchi, huku akisisitiza mtu akifanya kosa hilo lazima atakamatwa.
“Tunasema hivi, jambo lolote mhalifu anapolifanya lazima aache kitu cha kumtambulisha, kama kapita mlangoni lazima kuna kitu atakuwa kashika.
“Kama alihamisha fedha kwenda kwa mtu mwingine tunajiuliza hiyo namba ni ya nani na imesajiliwa kwa kitambulisho gani na cha nani.
“Kwa hiyo tunaamini kwamba, hakuna jambo mtu anaweza kufanya akakosa kutambuliwa, huwa tunawakamata na kuwachukulia hatua,” alisema waziri.