Dar es Salaam. Mshambuliaji Prince Dube bao lake dakika ya 90+4, lilitosha kuipa timu hiyo pointi moja ikiwa ni ya kwanza kwao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya TP Mazembe.
Hilo ni bao la kwanza kwa mshambuliaji huyo baada ya kupita takribani siku 91 tangu mara ya mwisho afunge Septemba 14, 2024 wakati Yanga iliposhinda 1-0 ugenini dhidi ya CBE SA hatua ya mtoano ya michuano hiyo.
Hata hivyo, ni bao lake la nne msimu huu katika michuano hiyo baada ya kufunga matatu hatua ya mtoano.
Dube amefunga bao hilo dakika ya mwisho ya mchezo akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa TP Mazembe, Alioune Badara Faty kufuatia shambulizi walilofanya Yanga.
Katika mchezo huo uliochezwa leo Desemba 14, 2024 kwenye Uwanja wa TP Mazembe jijini Lubumbashi nchini DR Congo, kikosi cha Yanga kilikuwa na mabadiliko ya wachezaji wawili kutoka kile kilichocheza dhidi ya MC Alger ambapo Khalid Aucho na Dickson Job walirejea wakichukua nafasi za Stephane Aziz Ki na Bakari Mwamnyeto.
Wenyeji TP Mazembe walionekana kuutaka zaidi mchezo huo kwani waliuanza kwa nguvu kubwa kiasi cha kwamba dakika mbili za kwanza walijikuta wakicheza faulo nne.
Hata hivyo, Yanga nayo ilikuwa imara kuzuia mashambulizi ya TP Mazembe waliokuwa wakitumia zaidi winga zao kutengeneza mashambulizi hasa upande wa kushoto alipokuwa akicheza Oscar Kabwit aliyekuwa akimsumbua Yao Kouassi huku shambulizi lake la dakika ya 17 likiishia mikononi mwa Djigui Diarra.
TP Mazembe walilazimika kufanya mabadiliko ya lazima dakika ya 21 baada ya Ousseini Badamassi kuumia na kutolewa, nafasi yake ikachukuliwa na Soze Zemanga.
Yanga ilipata pigo dakika ya 28 baada ya Djigui Diarra kuumia na kulazimika kutibiwa kwa takribani dakika tano, lakini aliendelea na mchezo huo. Hata hivyo, alishindwa kuendelea na kipindi cha pili, nafasi yake ikachukuliwa na Khomeiny Abubakar.
Dakika ya 42, Cheick Fofana aliyeingia muda mchache kuchukua nafasi ya Gloire Mujaya, aliifungia TP Mazembe bao kwa kichwa na kuipeleka timu yake mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Wakati kipindi cha pili kinatarajiwa kuanza, Yanga ilifanya mabadiliko ya wachezaji watatu, mbali na kuingia Khomeiny, pia Clement Mzize alichukua nafasi ya Maxi Nzengeli, wakati Mudathir Yahya akimpisha Aziz Ki.
Mabadiliko hayo yalionekana kutompa matokeo chanya ya haraka Kocha Sead Ramovic kwani baadaye dakika ya 61 akamtoa Kennedy Musonda na kuingia Prince Dube, kisha dakika ya 76 Duke Abuya alimpisha Clatous Chama.
Kidogo mabadiliko hayo yakaongeza uhai katika kikosi cha Yanga ambacho muda mwingi wachezaji walionekana kutocheza kwa mipango ya kusaka ushindi.
Kuingia kwa Chama, kuliongeza ubunifu eneo la ushambuliaji akishirikiana na Pacome Zouzoua, Aziz Ki, Clement Mzize na Dube.
Matokeo hayo pengine yameirudisha Yanga katika hesabu za kufuzu hatua ya robo fainali kwani itahitaji kushinda mechi tatu zilizobaki zikiwemo mbili nyumbani dhidi ya TP Mazembe na MC Alger na moja ugenini mbele ya Al Hilal.
Ikumbukwe kwamba, kabla ya mchezo huu, Yanga ilitoka kufungwa 2-0 na Al Hilal kisha matokeo kama hayo ikayapata mbele ya MC Alger.
Sare dhidi ya TP Mazembe imeendelea kuifanya Yanga kukaa mkiani mwa msimamo wa Kundi A la michuano hiyo ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi tatu.