Kwenye mahojiano ndani ya Mkutano wa 'The New York Times 2024 DealBoo' Jumatano, Prince Harry alikanusha uvumi unaodai ndoa yake na Meghan Markle ipo hatarini baada ya wawili hao kuhudhuria matukio tofauti kila mmoja akiwa kivyake.
“Tumeelezwa kuwa tumenunua au kuhama nyumba mara 10 au 12. Tumetalakiana mara nyingi pia, lakini kwa kweli, si hivyo,” alisema Harry kwa mshangao, akiongeza kuwa uvumi huo ni hatari na unamfanya kuwaza kwanini.
Pamoja na kuelezewa kuwa ana uzoefu mkubwa na vyombo vya habari, Harry aliwahurumia wale wanaoeneza uvumi, akisema: “Kwa kweli nahisi huruma kwa watu mtandaoni; matumaini yao yanajengwa kila mara halafu hayafikii ukweli.”
Harry na Meghan, waliooana mwaka 2018, hivi karibuni wameendelea kuwa gumzo kwa maamuzi yao ya kuhudhuria matukio kila mmoja akiwa peke yake. Hata hivyo, Harry alisisitiza kuwa ndoa yao bado ni imara, licha ya uvumi huo kusambaa mara kwa mara.
Wana watoto wawili, Archie mwenye umri wa miaka 5 na Lilibet mwenye umri wa miaka 3.