Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka 2024 yafanyike katika ngazi ya Mikoa huku akiagiza fedha zilizotengwa katika kila Taasisi kwa ajili ya maadhimisho hayo zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii.
Amesema kila Mkoa uhakikishe Wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira katika maeneo ya kijamii kama vile kwenye masoko, Hospitali, kambi za Wazee na wenye mahitaji maalum, mashindano ya michezo mbalimbali pamoja na makongamano na midahalo ya kujadili maendeleo endelevu ambayo Nchi imefikia katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru.
Amesema hayo leo Jumatano December 04, 2024 katika kikao kazi cha Mawaziri kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma ———> “Sherehe za mwaka huu hazitakuwa na gwaride na shughuli nyingine za Kitaifa”
Amesema Serikali inatoa wito kwa Wananchi kushiriki katika shughuli hizo ili kujivunia sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru wetu "Ninatoa rai kwa Wakuu wote wa Mikoa ya Tanzania Bara, kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo la kuuenzi Uhuru wetu”