RAIS wa Shirikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amesema anatamani kuiona Tanzania ikifika fainali ya michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Motsepe amesema hayo baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Tanzania akiwa katika ziara ya mataifa matatu ,Tanzania, Kenya na Uganda wenyeji wa CHAN 2025.
“Moyo wangu ukiwaza juu ya Tanzania, nakosa la kusema, natamani kuiona ikifika fainali ya CHAN,” amesema.
Motsepe amesema CHAN itakwenda kuwafungulia milango watu wengi, vijana kwa watoto kutimiza ndoto zao katika michuano hii ambayo Tanzania ni miongoni mwa nchi wenyeji.
“Sisi wote ni watoto wa baba mmoja Mwalimu Nyerere, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwenye kila kitu tangu miaka ya nyuma, kupitia Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace (Karia) soka limezidi kukua,” amesema.
Motsepe amesema anaamini CHAN itakuwa ya kiutofauti sana kwa kuwa inachezwa nchini Tanzania hivyo na Dunia nzima itashuhudia hilo.
Ameweka wazi kuwa baada ya kukagua Uwanja wa Benjamini Mkapa na kujiridhisha utatumika kwa mchezo wa kwanza wa sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo.
Baada ya kumaliza ziara katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam , Motsepe ameenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuangalia Uwanja wa New Amaan Complex baada ya hapo ataelekea nchini Uganda na Kenya.