Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, thamani ya Dola ya Marekani imepungua katika soko la fedha la kimataifa kiasi cha kuzua mjadala miongoni mwa wataalam wa masuala ya uchumi na fedha, huku baadhi wakitaja kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi kama kichocheo cha kuimarika kwa shilingi ya Tanzania.
Mtafiti wa masuala ya Fedha, ubalozi wa Tanzania Oman, Hashimu Mnubi anasema bidhaa za kilimo kama korosho na parachichi, pamoja na mauzo ya dhahabu, vimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Ripoti kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa katika mwaka ulioishia Julai 2024, Tanzania ilikusanya shilingi trilioni 34 kutoka kwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, ongezeko ambalo limeimarisha uthabiti wa shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Akizungumza kwenye mjadala wa Club House wa Diaspora, kujadili masuala ya uchumi na fedha, Mnubi amesema sekta ya utalii, ambayo ni mojawapo ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania, nayo imeonyesha ukuaji wa kasi.
“Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024 pekee, Tanzania ilivutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) wenye thamani ya dola bilioni moja za Marekani ikiwa ni ongezeko la asilimia 53 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana.” Amesema.
Ametaja sababu nyingine zilizochangia hatua hiyo ni mikakati thabiti ya kifedha inayotekelezwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaidia kudhibiti mfumuko wa bei, ambao umekuwa katika kiwango cha asilimia 3-5, kiwango kinachokubalika kimataifa kwa uchumi imara.
“Kupitia usimamizi makini wa mzunguko wa fedha, BoT imehakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na mazingira mazuri ya kiuchumi kwa wawekezaji wa ndani na nje. Hii imesaidia kuongeza imani ya wawekezaji na kuimarisha zaidi thamani ya shilingi,” amesema Mnubi.