Kamusi ya kiswahili sanifu inatafsiri neno DHARAU kama tabia ya kukosa kuthamini na kuheshimu mtu au watu. Kimsingi Yanga haithamini mashabiki wake. Nitakupa maelezo yakinifu juu ya hili..
November 18, 2024 Yanga ilimtangaza Abdihamid Moallin kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo. Ulikua ni uamuzi sahihi kwa sababu Yanga ilikua inakosa mtu wa kutengeneza sera za ufundi, muelekeo na falsafa ya soka la Yanga. Pia sina shaka na uwezo wa Moallin, CV yake imejitosheleza.
Baada ya Moallin kutangazwa kushika nafasi hiyo wiki kadhaa baadae Abdihamid Moallin anaonekana kama sehemu ya benchi la ufundi la Yanga kwenye mechi rasmi za klabu hiyo.
Wanaoruhusiwa kukaa kwenye benchi ni wachezaji wa akiba, makocha wasaidizi, Meneja wa timu, pamoja na madaktari wa timu. Lakini kumbuka Sead Ramovic alikuja na kocha wake msaidizi.
Kwa kuwa Mkurugenzi wa ufundi hastahili kukaa eneo la benchi la ufundi. Kitendo cha Moallin kukaa kwenye benchi la Yanga, kinaibua mjadala, Je Moallin anakaa kwenye benchi kama nani?
Mashabiki wa Yanga wanadharauliwa na Uongozi wa Yanga. Wameshindwa kuthaminiwa, na wamechukuliwa poa.
Mashabiki na wapenzi wa Yanga ambao wanalipia kadi za uanachama kwa mwaka mzima kwa pesa zao walizotolea jasho wanastahili haki zote za kupewa taarifa sahihi kwa wakati. Lazima waipate value of their hard earned money.
Yanga mpaka sasa haijatoa taarifa rasmi kama imembadilishia majukumu Moallin kutoka kuwa Mkurugenzi wa ufundi mpaka kuwa kocha msaidizi ambae anaonekana kwenye benchi.
Hizi ni dharau za wazi wazi wanazofanyiwa wapenzi na mashabiki wa Yanga. Ni muhimu Yanga kama taasisi iheshimu haki ya mashabiki wao kupewa taarifa sahihi na kwa wakati. Yanga iseme Moallin kabadilishiwa majukumu au la.