Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema matunda ya uwekezaji wa DP World katika Bandari ya Dar es salaam yameanza kuonekana ambapo katika kipindi cha miezi mitano tangu ianze kuendesha Bandari hiyo Serikali ya Tanzania imekusanya Tsh. bilioni 325
Akiongea Jijini Dar es salaam leo December 19,2024, Msigwa amesema “Tumeanza kuona matunda matamu ya DP World ndani ya kipindi kifupi sana, tangu kampuni ya DP World Dar es salaam ianze uendeshaji katika Bandari ya Dar es salaam mwezi April 2024, tumepata mafanikio yafuatayo, kwa mujibu wa mkataba kampuni ya DP World ambayo kwetu Tanzania inakuwa DP World Dar es salaam inapaswa kuwekeza USD mil 250 (Tsh.bilioni 675) katika kipindi cha miaka mitano, sasa katika kipindi cha miezi mitano tu tayari kampuni hii imeshawekeza Tsh. bilioni 214.425 na hii ni sawa na 31% ya uwekezaji tuliotarajia katika kipindi cha miaka mitano”
“Maana yake huko nyuma kulikuwa na maneno tumeweka Wasanii sijui nini watakuja sasa hapa kwa lugha ya Kikinga we mean business na tutasimamia mkataba huu kuhakiksha maslahi ya Watanzania yanalindwa”
“Ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA imefanyika na usimikaji wa mifumo ya TEHAMA ya uendeshaji wa Bandari umefanyika, sasa manufaa mengine ambayo wakati ule tuliyaimba sana tukaitwa Wasanii na mambo mengine mengi, wastani wa muda wa meli kusubiri wakati ule meli zetu zilikuwa zinasubiri siku 46 nyingine hadi siku 70 lakini sasa hivi meli zinasubiri kwa siku 7 maana yake tunapunguza gharama ambazo Serikali kupitia TPA imekuwa ikiwalipa wenye meli kutokana na meli zao kusubiri muda mrefu kushusha mizigo, na hiyo ni wastani lakini zipo meli hazisubiri kabisa, meli za makasha hakuna kusubiri zikija zinashusha zinaondoka”
“Tunaendesha bandari kwa faida, tulikuwa tunaendesha bandari kwa hasara, katika kipindi cha miezi mitano tangu DP World waanze kazi Serikali imefanikiwa kukusanya Tsh. bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingia kati ya TPA na DP World, haya ni maeneo ambayo tulipotoshwa sana tumeanza kupata faida”