Mmoja wa majeruhi waliopata ajali ya Coaster, Ally Hengo akiwa amelazwa wodi namba moja katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu. Picha Hamida Shariff
Morogoro. Majeruhi katika ajali iliyosababisha vifo vya watu 15 na wengine saba kujeruhiwa iliyotokea usiku wa kuamkia leo Desemba 18, 2024 eneo la Mikese, mkoani Morogoro amesimulia ilivyotokea.
Ajali hiyo ilihusisha basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster lililogongana na lori eneo la Mikese, barabara ya Morogoro - Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, chanzo cha ajali ni dereva wa lori lenye namba T 715 DZX lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kutaka kuyapita magari yaliyo mbele yake bila kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na Toyota Coaster likiwa na abiria lililokuwa likitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi, Awadhi Haji amesema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori ambaye pia amefariki dunia.
Amesema dereva huyo alitaka kuyapita magari ya mbele bila kuchukua tahadhari.
Ally Hengo, majeruhi wa ajali hiyo akizungumza na Mwananchi akiwa wodini katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro amesema alianza safari saa moja usiku akiwa kwenye Coaster.
Amesema walipofika Mikese alishuhudia dereva wa lori akiwa anayapita magari mengine, ghafla aligongana na Coaster hilo.
"Nilikuwa nimekaa mbele, nilipoona dereva wa lori amezidi upande wetu nilijikuta nimeinuka na kugeuka nyuma, nilisikia kishindo na baadaye nikajikuta nimebanwa na siti. Hali niliyokuja nayo hapa hospitali haikuwa nzuri, lakini matibabu niliyopata kwa sasa naendelea vizuri," amesema Hengo.
Amesema ndugu zake wameshapata taarifa na wamefika hospitalini hapo. Amewashukuru madaktari kwa huduma bora na ya haraka waliyompatia na Jeshi la Polisi, kwani askari walifika haraka eneo la ajali na kutoa msaada.
Magari yaliyopata ajali kwa kungona yakiwa eneo la Mikese, Barabara ya Morogoro - Dar es Salaam.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Desemba 18, Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Daniel Nkungu amesema miili mitano imeshatambuliwa na ndugu, huku majeruhi saba wakiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Dk Nkungu ametaja majina ya miili iliyotambuliwa kuwa ni ya Rashid Mtafya, Kisonda Ndaluma, Juma Hassan, Hamza Ally na Mohamed Kollo, aliyekuwa dereva wa lori lililosababisha ajali.
"Mpaka sasa hakuna majeruhi yeyote aliyehamishwa, wote wapo hapa wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinazidi kuimarika, wengi wamepata mivunjiko ya miguu, mikono na nyonga. Hakuna majeruhi anayehitaji kufunguliwa kichwa," amesema.
Amesema uongozi wa hospitali umeweka utaratibu mzuri wa kutambua miili ya marehemu, hivyo amewataka wananchi wenye wasiwasi na ndugu zao kufika mochwari kuitambua.
"Kwa utaratibu wa hospitali, miili huwa inakaa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa siku 14 baada ya hapo kama haitatambuliwa itazikwa kwa utaratibu wa sheria iliyopo," amesema.
Nyuso za huzuni ndizo zilionekana eneo la mochwari, baadhi wakiangua vilio baada ya kutambua miili ya wapendwa wao.
Wengine walionekana wakifanya utaratibu wa kupata majeneza ili kwenda kuichukua miili hiyo.
Ili kukabiliana na ajali za barabarani, Kamishna Awadhi amesema: "Jeshi la Polisi tutafanya oparesheni kuyakamata magari mabovu yanayotembea barabara ambayo abiria wamekuwa wakiyapanda wa kile wanachodai ni shida ya usafiri na baadaye magari hayo kusababisha ajali.
"Abiria watakaozidi kwenye vyombo vya usafiri kupitia oparesheni hii nao tutawashusha, tunaomba abiria mtuvumilie," amesema.
Amewataka madereva kuchukua tahadhari hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya.
Awadhi amesema dereva atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua za kisheria.