Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga Chido katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar.
Taarifa ya TMA ya leo Desemba 12, 2024 iliyopo kwenye tovuti yake imesema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku nne zijazo (Desemba 13 hadi 16, 2024).
TMA imesema kwa sasa kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja Tanzania.
Hata hivyo, TMA imesema kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga Chido kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa Tanzania, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo jirani hususan kati ya Desemba 14 na 16.
“Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalamu wa kisekta,” imeshauri TMA.
Imesema inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.
Wakati huohuo, utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo Desemba 12 uliotolewa na TMA unaeleza mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu itakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Kwa upande wa Visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Singida, Dodoma, Dar es Salaam na Tanga, kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro; mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Pwani (ikijumuisha Visiwa vya Mafia), Rukwa, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe itakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Kwa upande wa kusini mwa Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara itakuwa na hali ya mawingu kiasi na vipindi vya jua.
Kuhusu upepo wa pwani, TMA imesema unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa kwa pwani yote. Kutoka kaskazini mashariki kwa pwani ya kaskazini na kutoka kaskazini kwa pwani ya lusini.
TMA imesema hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi madogo.
“Matarajio kwa siku ya Jumamosi Desemba 14, mabadiliko kidogo,” imesema TMA katika taarifa.