TOTO Afya Kadi inarejea. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kuanzia Januari mwakani, watoto wenye umri usiozidi miaka 21 watanufaika nayo.
NHIF ilisitisha Toto Afya Kadi mwaka jana baada ya kubainika ilikuwa inasababisha hasara kubwa kwa mfuko kutokana na kundi hilo kutumia zaidi ya kile ilichokuwa inachangia kwa mfuko.
Vilevile, uongozi wa mfuko huo umesema umeokoa Sh. bilioni 5.44 kwa kipindi cha Julai 2023 hadi 2024 kutokana na kuzuia mianya ya udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya wanachama na vituo vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza jana jijini Dodoma na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk. Irene Isaka alisema wamefunga mifumo thabiti kudhibiti udanganyifu ambao ulifanywa na wanachama, watoa huduma na madaktari.
Dk. Isaka alisema mfuko huo unaelemewa na makundi matatu ambayo ni wenye umri mkubwa, wenye magonjwa yasiyoambukiza na Toto Afya Kadi.
Alisema kwa kipindi cha miaka saba kuanzia 2016/17 hadi 2023/24 cha huduma hiyo, walipata hasara ya asilimia 366 kulinganishwa na fedha ambazo wanufaika hao walichangia kwa mfuko.
Dk. Isaka alitolea mfano wa mwaka 2023 ambao wanufaika 185,021 walichangia Sh. bilioni 10.134 lakini walitibiwa na mfuko kwa gharama ya Sh. bilioni 31.764 sawa na hasara ya asilimia 313.
Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama wa NHIF, Hipoliti Lelo, alisema mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote umeondoa sharti la kufikisha idadi ya wanafunzi 100 ndipo wasajiliwe kuwa wanachama na kupata huduma.
Lelo alisema kwa sasa shule au chuo kinaweza kusajili wanafunzi waliopo wasio na huduma hiyo na wakapewa huduma bila kujali idadi.
"Mfano, shule ina wanafunzi 80 halafu 20 wana bima, wale 60 waliobaki tutawasajili. Au wazazi wanasuasua kujiandikisha na tayari kuna wachache wako tayari, tutawasajili na wataendelea kuwa wanachama na kupata huduma," alisema.
Alisema utaratibu wa kuandikisha umeanza kwenye vyuo mbalimbali kwa wote wenye umri wa miaka 18 na kwamba wanaweza kujisajili moja kwa moja wenyewe.
UDANGANYIFU
NHIF imeokoa Sh. bilioni 5.44 kwa kipindi cha Julai 2023 hadi 2025 kutokana na kuzuia mianya ya udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya wanachama.
Dk. Isaka alisema wamekutana na matukio ya kadi ya mwanafunzi kutumiwa na watu watatu kujifungua ndani ya mwaka mmoja, na baada ya uchunguzi ilibainika aligawa kadi kwa watu wengine.
Pia wamebaini mwanachama kwenda kutibiwa malaria kisha kupewa vipimo na dawa nyingine ambazo hazihusiani na matibabu aliyoyapata.
"Tumekutana na matukio mtoto ameenda kufanyiwa tohara, lakini kalazwa kwa siku tatu, wakati ni huduma anayoipata kwa saa chache na kuondoka ila alilazwa kusubiri siku ya kutahiriwa kisha akafanyiwa na kupumzishwa siku ya tatu akaruhusiwa. Hii si sawa kwa kuwa ni huduma unayopata kwa saa chache na kuruhusiwa," alisema.
Alisema hatua zilizochukuliwa, kadi 12,685 zilifungiwa kutokana na udanganyifu, mikataba 11 ya watoa huduma imesitishwa na hivyo kufanya jumla ya mikataba 55 iliyositishwa tangu mwaka 2018.
Alisema watumishi watatu wa mfuko wamechukuliwa hatua za kinidhamu baada ya mashauri yao kukamilika na wengine wanane taratibu zinaendelea na hivyo kufanya jumla ya watumishi 11 waliochukuliwa hatua za kinidhamu.
Dk. Irene alisema watumishi wa sekta ya afya wapatoa 36 taarifa zao zimewasilishwa katika mamlaka za kinidhamu.
UHAI WA MFUKO
Dk. Irene alisema uhai wa mfuko mwaka 2001/02 ulikuwa miaka saba na miezi tisa lakini ukashuka hadi miezi sita Juni mwaka jana, na ulipanda hadi mwaka mmoja Juni 2024.
Alisema makusanyo hadi Juni 2024 ni Sh. bilioni 756.48 sawa na asilimia 101.3 ya lengo la kukusanya Sh. bilioni 746.76.
Alisema asilimia 26.4 ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Kati yao, asilimia 70 wako vijijini, wote wanastahili kupewa bima bila kuchangia.
Kwa mujibu wa Dk.Irene, kuna ongezeko kubwa la wazee wa kuanzia umri wa miaka 60 ambao wana changamoto kubwa za afya, hasa magonjwa yasiyoambukiza.
Alisema vituo vya kutolea huduma za afya vyenye mkataba na NHIF na kiasi cha asilimia kwenye mabano ni serikali (73), sekta binafsi (18) taasisi za dini (9).
Alisema kwa kipindi cha kuishia Juni 2024 mfuko umelipa madai ya vituo vya kutolea huduma ya Sh.bilioni 650.4, ikiwa ni asilimia 37 vya serikali, 35 binafsi na 28 vya madhehebu ya dini.
WASTAAFU
Kuhusu kundi la pili linalochangia hasara kwa mfuko, Dk. Irene aliwataja wastaafu ambao waliongezeka kutoka 151,500 mwaka 2021/22 hadi 152,000 katika miaka iliyofuata hadi 2024.
Alisema hata idadi ya wagonjwa kutoka kundi hilo iliongezeka kutoka 36,936 mwaka 2016/17 hadi 125,582 mwaka 2021/22 kabla ya kushuka hadi 120,551 mwaka 2023/24.
Alisema hata wastani wa mahudhurio yao hospitalini ulipanda kutoka matatu 2016/17 hadi saba mwaka 2020/21 na miaka iliyofuata, hali inayoonesha ongezeko kubwa la matibabu kwa kundi hilo.
"Ongezeko kubwa la malipo ya gharama za matibabu kwa kundi hilo lilikuwa ni mwaka 2017/18 la asilimia 58, na asilimia 43 mwaka 2018/19. Pia kumekuwa na ongezeko la gharama kwa asilimia 22 mwaka 2022/23 na asilimia tano mwaka 2023/24, wakifikia kiwango cha juu cha malipo cha Sh. bilioni 91.9," alifafanua.
MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Dk. Irene alisema magonjwa yasiyoambukiza yanaugharimu mfuko mabilioni, akisisitiza kuwa kuna ongezeko kubwa la wanufaika wanaougua magonjwa hayo na kwamba si wenye umri mkubwa pekee bali umri mwingine.
"Nikiona duka la pombe, mapigo ya moyo wangu yanaongezeka. Magonjwa yasiyoambukiza yanaugharimu sana mfuko. Tuelimishe jamii itumie vinywaji hivyo pasi na kuathiri afya," alisema.
Naye Lello alisema Bima ya Afya kwa Wote inapoanza kwa sasa wanachama watatumia Kitambulisho cha Taifa kupata huduma.
Alisema taasisi za umma ambazo serikali ina hisa asilimia 30 ni lazima kuingia kwenye utaratibu, na kwamba kutakuwa na skimu binafsi kwa kampuni na taasisi binafsi.