Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (@ChademaTz) Bara, @TunduALissu, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho ngazi ya Taifa, ametoa wito kwa Mwenyekiti wa sasa @freemanmbowetz, kueleza kwa uwazi kuhusu madai ya kutumia mabilioni ya fedha ndani ya chama.
Akizungumza kupitia mtandao wa kijamii wa Clubhouse, Lissu amesema kuwa, Mbowe amekuwa na mchango mkubwa kwa chama kwa kusaidia kifedha, ikiwemo kutoa mikopo iliyosaidia kufanikisha shughuli mbalimbali za chama.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kila matumizi ya fedha ndani ya chama yanapaswa kuwa na nyaraka za kuthibitisha.
“Ni kweli mwenyekiti wetu Mbowe amekisaidia sana chama. Alitukopesha fedha na tukazilipa kupitia ruzuku za chama. Hata chopa tulizoamua kama chama zitumike, tulishalipa zote,” alisema Lissu.
Lissu ameongeza kwa kusema kuwa, hana taarifa za kina kuhusu madai ya mabilioni yaliyotumika zaidi ya gharama zilizojulikana na kukubaliwa na chama.
“Sasa nasikia kuna mabilioni ametumia, sijui ni yapi hayo. Lakini ninavyojua, gharama zililipwa kutokana na kile tulikubaliana kama chama,” alibainisha.
Akizungumzia uwazi wa matumizi ya fedha za chama, Lissu amesisitiza kuwa hakuna fedha inayoweza kutumika bila nyaraka za kuthibitisha.
“Kama kuna mtu ameweka mabilioni kwenye chama, atoe document kuhusu hizo fedha. Hakuna fedha isiyo na document, hakuna fedha ya chama isiyo na document,” alisema kwa msisitizo.
Lissu pia ameeleza kuwa mbali na Mbowe, wanachama wengine wengi wamejitolea na kuwekeza katika chama kwa njia mbalimbali. Hata hivyo, alifafanua kuwa mikopo yote iliyochukuliwa imekuwa ikilipwa kwa uwazi na kufuata makubaliano ya chama.
“Hata sisi wengine tumewekeza kwenye hiki chama. Watu wengi wamekitumikia chama kwa hali na mali, lakini fedha za kukopwa zimelipwa,” aliongeza.
Kauli ya Tundu Lissu inadhihirisha umuhimu wa uwajibikaji wa viongozi katika kudumisha imani ya wanachama na wananchi kwa ujumla kwa kusisitiza uwazi kuhusu matumizi ya fedha huku akisisitiza kwamba mafanikio ya chama yanapaswa kujengwa juu ya misingi ya uadilifu na ukweli.