Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (@ChademaTz) na mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho ngazi ya Taifa, @TunduALissu, ameeleza kushangazwa na hatua ya Mwenyekiti @freemanmbowetz kuandaa tuzo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. @SuluhuSamia bila kushirikisha kamati kuu ya chama hicho.
Akizungumza kupitia mtandao wa Clubhouse usiku huu, Lissu ameeleza kuwa Rais Samia alialikwa na Mbowe kushiriki katika mkutano wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA), na walijulishwa tu kuwa mwaliko huo umetoka kwa Mwenyekiti.
Ameongeza kwa kusema kuwa, walishangaa kuona tuzo ikitolewa kwa Rais Samia bila kujulishwa mapema, huku kamati kuu ya chama hiyo ikiwa haijakaa kujadili suala hilo.
"Yalikuwa ni maamuzi ya Mwenyekiti pekee yake kwa haya mambo mawili. Hakuna kikao kilikaa kamati kuu kumwalika Rais Samia au kumpa tuzo," alisema Lissu, akimtaka Mwenyekiti Mbowe kuhojiwa kwa nini alitoa tuzo hiyo na kumleta Samia, wakati chama cha CCM kilikuwa hakijakubali chochote kuhusu maridhiano kati ya pande hizo.
Lissu amekumbusha kwamba masharti ya mwanzo ya maridhiano kati ya CHADEMA na Serikali yalikuwa na vipengele maalum, na kwamba anajiuliza ikiwa hatua ya kutoa tuzo kwa Rais Samia ni matokeo ya maridhiano hayo.?
Tuzo hiyo, aliyopewa Rais Samia Suluhu Hassan, ilitolewa na Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) mnamo Machi 08, 2023, kwa kumpongeza kwa juhudi zake za kuboresha na kuimarisha demokrasia nchini, huku akihusishwa na amani, upendo, na mshikamano.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Rais Samia na Mwenyekiti Freeman Mbowe kwa niaba ya BAWACHA wakati wa Kongamano la Siku ya Wanawake lililofanyika mjini Moshi.