Uamuzi Kuntu wa Tundu Lissu Waibua Minyukano Mitandaoni

Uamuzi Kuntu wa Tundu Lissu Waibua Minyukano Mitandaoni


Dar es Salaam. Joto la uchaguzi wa Chadema ngazi ya taifa, limepamba moto katika mitandao ya kijamii.


Baada ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kutangaza nia ya kuwania uenyekiti wa Taifa, imeshuhudiwa minyukano ya makada na hoja zenye mitazamo tofauti za wadau wa siasa, wanaharakati na wananchi.


Kwa upande mmoja, uamuzi huo umepokelewa kama usaliti kwa baadhi ya makada wa chama hicho, huku wengine wakionyesha kufurahishwa, wakiuhusisha na kukomaa kwa demokrasia ndani ya Chadema.


Kundi linaloutafsiri uamuzi huo kama usaliti kwa linajenga hoja kuwa unaweza kukipasua chama, hivyo alipaswa kuacha nafasi hiyo iendelee kushikiliwa na aliyepo sasa, Freeman Mbowe na yeye aendelee na umakamu uenyekiti bara.


Lakini wale wanaomsifu, wanasema alichokifanya kinathibitisha kukomaa kwa demokrasia na kuzingatiwa kwa Katiba ya chama hicho inayompa haki mwanachama yeyote kugombea.


Kadhalika, wapo wanaofurahishwa wakimwona Lissu kama tumaini jipya na kuwa ndiye atakayefanikisha mageuzi ndani ya chama hicho na hatimaye kishike dola, wakidai miaka 20 imetosha kwa Mbowe kuiongoza Chadema.


Lissu mwenyewe akizungumzia vijembe anavyopigwa mitandaoni alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Jumanne Desemba 10, 2024, makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, alisema haogopi.


“Jamani mimi natembea na risasi mgongoni, sawa? Nitaogopa mawe ya mitandaoni, eeh..? Natembea na risasi iko hapa, nitaogopa nani?” alisema akishika eneo la mgongoni.


Hata baada ya kauli hiyo, minyukano imeamshwa upya baada ya tangazo lake la Alhamisi Desemba 12.




‘Ukipigwa usihame chama’


Mmoja mwa makada wanaotajwa kuwa upande wa Mbowe, Boniface Jacob, ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, muda mfupi baada ya mkutano wa Lissu, aliandika kwenye ukurasa wake wa X akisema:


“Ndugu yako akitaka kupigana vita na wewe, mkatalie na umsihi sana asitoe upanga ndani ya ala yake. Asiposikia akataka vita zaidi, muitie ndugu wengine na wazee wa ukoo wamsihi umuhimu wa umoja wa familia.


 “Asipowasikiliza ndugu zake, wazee na majirani, muitie viongozi wa dini na wazee wamsihi madhara ya vita. Akiwakatalia wote hao, mpe anachokitaka (vita). Usimuonee huruma kabisaaaaa. Na iwe funzo kwake na ndugu wengine kuwa umoja na upendo katika familia yenu ni muhimu kuliko tamaa binafsi.”


Kauli nyingine inayoaminika kumtahadharisha Lissu imetolewa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi akiandika; “Ifahamike kuwa; wajumbe wa Mkutano Mkuu Chadema Taifa ni zaidi ya 1,200. Ubwabwa wa kushiba huonekana kwenye sahani.


“Tukubaliane, ukipigwa hakuna kuhama chama wala kujiliza! Don't hate the players, hate the game! (usiwachukie wachezaji, uchukie mchezo).”


Hata hivyo, makada wengine wa Chadema hawakuonyesha kuegemea kwenye upande wowote katika maoni yao, akiwamo Martin Maranja Masese ambaye katika ukurasa wake wa X, amekisifia chama chake.


 “Chadema ni chama chenye mvuto katika jamii. Uchaguzi wa mwenyekiti unajadiliwa na kufuatiliwa na makundi rika tofauti katika jamii. Hakika, tunakwenda kuwapa uchaguzi bora wa ushindani. Siyo chaguzi za CCM, mwenyekiti anagombea na kivuli. Fomu moja kama hati ya kifo,” ameandika.


Ujumbe huo ulifuatiwa na mwingine aliondika, “mijadala ya uchaguzi wa Chadema imeshika hatamu. Hata CCM na vyama vingine vya mfukoni wanajadili uchaguzi wa Chadema.


“Hii ni uthibitisho kwamba chama chetu sasa ni kikubwa sana katika jamii. Tunataka mijadala iwe Chadema hadi mwaka kesho. Uchaguzi wetu utafanyika Januari 2025,” ameandika.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amendika katika mtandao huo, akitaka watu watofautishe uamuzi wa Lissu na utovu wa nidhamu.


“Kuna tofauti kubwa kati ya minyukano na utovu wa nidhamu. Jambo la msingi ni kuwa wanachama wetu wengi pengine watakuwa wanajua tofauti zake.


“Utovu wa nidhamu unaua umoja na upendo na mahusiano. Tuko katika kipindi cha kawaida sana cha kisiasa ndani ya chama chetu, isipokuwa kwa namna tunavyotazama, kufikiri, kutenda ndio linaweza kuwa tatizo au baraka,” ameandika.


Mbali na makada wa Chadema, wanaharakati kadhaa nao wametia maneno kwa uamuzi huo wa Lissu.


Mwanaharakati, Tito Magoti alitumia mtandao wa X kuwakosoa wanaomzodoa Lissu:


“Kujimilikisha usahihi, busara na zaidi ni uhayawani. Ondoka gizani na uikubali demokrasia au amua kuacha kabisa, ukavue samaki Ukerewe,” ameandika.


Amesema unaweza kuwa na maoni kuhusu Lissu, lakini wakati wote unapaswa kutambua kuwa demokrasia ni gharama.


“Ni muhimu kwa mashujaa wa demokrasia kuelewa masharti yake ya msingi, kumshambulia Lissu kwa kuwasilisha azma yake ya kuongoza Chadema haina maana. Hii si vita. Ni maendeleo. Kubali mchakato huu.”


Ujumbe za kuunga mkono uamuzi wa Lissu umechapishwa pia na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi aliyesema anahitaji wanasheria thabiti wengi zaidi kushiriki katika michakato ya kisiasa ndani ya vyama na nje.


“Kuwa na ushindani wa haki ndani ya vyama vya siasa ni njia ya kuheshimu michakato ya kidemokrasia nje ya vyama. Kila la kheri Tundu Lissu unastahili na upate.”


Mwanaharakati wa mitandaoni Maria Sarungi pia amemuunga mkono Lissu akiandika amekutana naye miaka 10 iliyopita na aliitwa majina mabaya na wabunge wa CCM, lakini alibaki na misimamo na nguvu yake ileile.


“Pindi niliposimama katika Bunge Maalumu la Katiba kupinga jaribio la CCM kubaribu Katiba ya wananchi iliyoandikwa na Tume ya Jaji Warioba, naye (Lissu) alikuwa akiniita jina baya nilikuwa nakataa mwanzoni, lakini baadaye tukawa tunafurahia,” ameandika.


Amesema kuanzia wakati huo, vyovyote utakavyomwita yeye au Lissu, isingewezekana kuwaondoa katika msimamo wa jambo wanaloliamini.


Amesema watu wanahitaji mabadiliko ya msingi, mfumo na mabadiliko ya jumla.


“Mtu anayejiamini kutuongoza katika mabadiliko hayo muhimu ni Tundu Lissu,” amesema.


Vijembe pia vilishuhudiwa katika mtandao huo, kikiwemo kile kilichoandikwa na Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo, “kawashika pazuri. Pale ambapo silaha inamgeukia mwenye silaha! Nimekaa paleee!”


Mdau mwingine wa siasa, Dk Chris Cyrilo kupitia ukurasa wake wa X, ameandika: “Nafasi ya uenyekiti taifa kwa CCM haigombewi. Hii inatunyima nafasi nzuri ya kujifunza demokrasia kutoka CCM, labda tujifunze kwa Chadema. Lakini kama wanaotaka uenyekiti wanafanya jambo hilo kama vita, na endapo wanaokalia kiti watafanya vita kubakia kitini, basi hatutajifunza kitu.”


Kwa upande wa Dedan Chacha Wangwe, ameandika ushindani ndani ya chama ni jambo la kikatiba na haki ya kila mwanachama.


“Rai yangu kwa viongozi na wana-Chadema, hasa vijana, tuweni makini katika ushindani huu wa ngazi ya kitaifa unaotarajiwa. Vinginevyo waathirika wakubwa tutakuwa sisi ambao safari yetu ya kisiasa bado ni ndefu,” ameandika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad