HESABU za Yanga kwa sasa hazipo sawa baada ya kupoteza mechi ya pili ya Kundi A katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikitishia tumaini la kucheza robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo, lakini tayari mabosi wa klabu hiyo akiwamo Kocha Sead Ramovic wamepanga kufanya uamuzi mgumu kwa timu hiyo.
Yanga ilipoteza mchezo wa pili ikiwa ugenini mjini Algiers, Algeria ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa MC Alger, ikiwa ni wiki moja tangu iliponyukwa kwa idadi kama hiyo na Al Hilal ya Sudan na kuiacha ikiwa mkiani mwa kundi hilo bila ya pointi wala bao lolote la kufunga na ikiruhusu kufungwa mabao manne.
Mara baada ya pambano hilo lililopigwa juzi usiku kwenye Uwanja wa Uwanja wa July 5, mabosi wa timu hiyo waliamua kuitisha kikoa cha dharura na kocha Ramovic, kisha kuanza kuchora ramani nzito ambayo kama ikifanyika tu, itakuwa kama kikosi hicho kimefumuliwa na kuanza hesabu mpya.
Yanga inaona ili kikosi hicho kirejee katika makali yanayohitajika, basi kuna wachezaji wapya sita wanahitajika haraka kurudisha makali yao ya miaka mitatu mfululizo walipokuwa tishio ndani na nje ya nchi.
ENEO LA ULINZI
Katika hesabu hizo, Yanga inataka kuanza na eneo la ulinzi ikianzia kwa kipa na licha ya ubora wa Djigui Diarra, lakini atasakwa kipa mwingine atakayekuja kurudisha ushindani zaidi.
Hesabu hizo za eneo hilo la makipa huenda likamweka kwenye wakati mgumu Aboutwalib Mshery ambaye amekuwa akikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara mbele ya Abubakar Khomeny na Diarra.
Mbali na makipa pia Yanga itarudi sokoni kusaka beki wa kati mwenye ubora kama wa Ibrahim Bacca au Dickson Job usajili uliotajwa mara tu baada ya kocha mpya Sead Ramovic kutua klabuni hapo.
Kocha huyo pia anataka kuona analetwa beki wa kushoto atakayekuja kushindana na Mkongomani Chadrack Boka kufuatia Nikson Kibabage kuonyesha wasiwasi wa kuziba nafasi hiyo kwenye mechi alizocheza wakati mwenzake akiwa majeruhi.
Boka huenda akarudi kazini kuanzia mchezo ujao baada ya kupona majeraha yake yaliyomuweka nje kwa takribani mwezi mzima.
VIUNGO WAWILI
Hesabu hizo mpya za Yanga ambazo Mwanaspoti imezinasa zimehitaji pia kiungo mkabaji mwenye nguvu baada ya Khalid Aucho kuonyesha wasiwasi kufuatia majeraha akiwa anarejea akianza kupona sawasawa.
Tangu Aucho aumie Yanga hivi karibuni imekuwa ikiwatumia Duke Abuya na hata, Maxi Nzengeli kuweka uzito wa eneo hilo lakini bado kumekuwa na nafasi kwa wapinzani kufika kirahisi kwa mabeki wa kati wa timu hiyo.
Ukiacha nafasi ya kiungo mkabaji pia ripoti hiyo inahitaji winga mwenye asili ya mguu wa kushoto atakayekuja kuirudishia uhai nafasi ya kiungo mshambuliaji wa kushoto.
Eneo hilo sasa limekuwa likitumikiwa na viungo wa kati Clatous Chama, Maxi na hata Pacome Zouzoua wakipishana kulingana na mfumo unaotakiwa kutumika.
MCHANA NYAVU
Ripoti hiyo pia imeonyesha mahitaji ya mshambuliaji wa kati mwenye makali atakayekuja kusaidiana na Kennedy Musonda ambaye angalau ameonekana kueleweka na kocha Ramovic.
Msako wa mashine hizo Mwanaspoti unafahamu umeshaanza kimyakimya tena kwa haraka ukisimamiwa na kocha wao Ramovic na mabosi wasiozidi wanne wa timu hiyo.