Baada ya Kufuzu Robo Fainali CAF Kibabe, Mchongo wa Kufika Nusu Fainali Wawekwa Wazi

Baada ya Kufuzu Robo Fainali CAF Kibabe, Mchongo wa Kufika Nusu Fainali Wawekwa Wazi


SIMBA SC imefuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kibabe baada ya kuifunga CS Constantine ya Algeria mabao 2-0, na kuongoza kundi A kwa kufikisha pointi 13 ikiwaacha Waarabu hao nafasi ya pili na pointi 12.

Katika kundi hilo, Simba na Constantine zimetinga robo fainali huku Bravos ya Angola ikimaliza ya tatu na pointi saba, wakati CS Sfaxien kutoka Tunisia ikiburuza mkiani baada ya kukusanya pointi tatu.

Kitendo cha Simba kuongoza kundi, kinaifanya kukutana na timu zilizomaliza nafasi ya pili makundi mengine ya B, C na D.

Stellenbosch ya Afrika Kusini iliyomaliza nafasi ya pili kundi B na pointi tisa, nyuma ya mabingwa wa michuano wa hiyo 2019-2020 na 2021-2022, RS Berkane ya Morocco, inaweza kukutana na Simba robo fainali.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Steve Barker, inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza katika historia yake, hivyo inaweza ikawa faida kwa Simba ambayo imekuwa na uzoefu mkubwa, japo inapaswa kujipanga ili kutinga nusu fainali.

Timu hii ilifuzu michuano hii baada ya kutwaa ubingwa wa Carling Knockout Cup huko Afrika Kusini huku ikiwa tishio baada ya kuzifunga timu mbalimbali maarufu zikiwemo Orlando Pirates, Chippa United na Amazulu.

Ikiwa Simba itapangiwa na Stellenbosch FC, itakuwa mara ya pili kwa misimu ya karibuni kukutana na timu kutoka Afrika ya Kusini, baada ya kutokea msimu wa 2021-2022, ilipokuwa pia Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa na Orlando Pirates.

Simba ilitolewa na Orlando Pirates hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya kushinda Kwa Mkapa 1-0, Aprili 17, 2022, kisha kwenda Afrika Kusini na kuchapwa pia bao 1-0, Aprili 24, 2022.

Timu nyingine ambayo inaweza kukutana na Simba ni ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliyomaliza ya pili katika kundi C na pointi nane nyuma ya mabingwa wa michuano hiyo msimu wa 2022-2023, USM Alger ya Algeria iliyoongoza na pointi 14.

ASEC sio wageni wa Simba kwa sababu timu hizo zimekutana mara sita katika michuano ya Kimataifa ambapo mbili ni Kombe la Shirikisho na minne Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kila mmoja ikishinda miwili, sare miwili na kupoteza miwili.

Miamba mingine ambayo Simba inaweza kupangiwa nayo ni Al Masry ya Misri iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kundi D, nyuma ya wapinzani wao kutoka nchi moja, Zamalek ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo wakichukua msimu wa 2023-2024.

Zamalek iliyotwaa ubingwa huo msimu uliopita na ule wa 2018-2019, ilimaliza kinara wa kundi D na pointi 14 na kuiacha Al Masry ambayo inatoka pia Misri kumaliza ikiwa nafasi ya pili, baada ya kujikusanyia ponti tisa.

Kitendo cha Al Masry kumaliza nafasi ya pili kinaweza kuifanya kukutana na Simba ambapo ikiwa zitakutana itakuwa ni mara ya tatu kwao katika michuano ya kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni, baada ya miamba hiyo kukutana pia mwaka 2018.

Timu hizo zilikutana raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mechi ya jijini Dar es Salaam ilikuwa sare ya mabao 2-2, Machi 7, 2018, kisha marudiano Misri zikatoka suluhu (0-0), Machi 17, 2018, na Simba kutolewa kwa mabao ya ugenini.

Moja ya faida kubwa kwa Simba ni kumaliza kinara ambapo hatua ya robo fainali itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani kwa mujibu wa kanuni ya 3(24), inayofafanua: “Washindi wa pili watacheza mechi zao za kwanza za robo fainali nyumbani.”

Faida nyingine kwa Simba ni kukutana na timu ambazo si ngeni na hazijawahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo tofauti na ilivyokuwa kwa vigogo vingine wakiwemo mabingwa watetezi Zamalek (Misri), USM Alger (Algeria) na RS Berkane (Morocco).

Akizungumzia hatua hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids alisema ni jambo nzuri kumaliza nafasi ya kwanza ingawa hatua iliyopita ni tofauti na inayokuja, hivyo benchi la ufundi linajipanga vyema kwa changamoto mpya ijayo.

“Moja ya malengo yetu yalikuwa ni kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi na tumefanikiwa kwa hilo, hatua inayofuata ni kama tunaanza tena upya na kilichotokea mwanzoni tumeshaachana nacho na tunasubiria kujua mpinzani wetu atakayekuja,” alisema Fadlu.

Kwa upande wa kinara wa mabao ndani ya Simba hatua ya makundi, Kibu Denis aliyefunga matatu, amesema  kuwa haikuwa rahisi kufuzu robo fainali na kuongoza kundi, hivyo kwa sasa wanajipanga kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa michuano hiyo.

“Tumeweza kutoboa hatua ya mtoano na makundi, sasa tumetinga robo fainali, zote zilikuwa ngumu, tunapoenda ndio kuna ugumu zaidi, mipango yetu ni kuona tunaweka rekodi nyingine kubwa ya kutwaa taji,” alisema.

“Hakuna kisichowezekana, kila mipango tuliyoipanga kuanzia hatua ya awali hadi sasa tumeifanikisha kwa usahihi, naamini hata hatua inayofuata tunaweza kuipambania na hatimaye kuandika historia ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho.”

Akizungumzia ubora wake, Kibu alisema: “Haya ni mashindano ya muda mfupi, ukifanya kosa moja umepoteza tofauti na ligi unaweza ukakosea mechi mbili unajua utapambana kwenye mechi 14 na zaidi zijazo, nafurahi nafanya kazi yangu kwa usahihi kwenye nyakati sahihi nikiisaidia timu yangu kufikia malengo.

“Licha ya kutokuwa bora Ligi Kuu Bara naamini pia nina nafasi ya kusawazisha makosa na kuwa bora kama ilivyo kwenye michuano hii ambayo bado tuna nafasi ya kuendelea kuipambania bendera ya nchi lakini pia timu kwa ujumla tuweze kuandika historia.” Simba imetinga hatua ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu 2018-2019, ikiwemo mbili ya Shirikisho Afrika na nne Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa kinara wa kundi kwa mara ya pili.

Mara ya kwanza Simba kuongoza kundi ilikuwa msimu wa 2020-2021, iliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza kinara wa kundi A ikikusanya pointi 13, ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri iliyomaliza ya pili na pointi 11.

AS Vita Club ya DR Congo ilimaliza ya tatu na pointi saba, huku Al Merrikh ya Sudan ikiburuza mkiani na pointi mbili tu, ambapo msimu huo Simba iliishia robo fainali baada ya kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad