BERNARD Morrison alikuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Songwe wikiendi iliyopita akisaini katika klabu ya KenGold ya pale Chunya Hapana shaka baada ya kutua viwanja vya Songwe alipita kando ya Uwanja wa Sokoine na kuanza kupandisha vile vilima vya kuelekea Wilaya ya Chunya.
Kutoka Soweto hadi Chunya. Kutoka uzunguni mwa Jiji la Johannesburg pale Sandton kisha hadi Chunya, Mbeya. Nadhani ni maisha ambayo Morrison amejichagulia mwenyewe. Tusimuingilie sana. Tusimvurugie sana alichopangamaishani. Kupanga ni kuchagua. Nadhani yeye amechagua kuwa kama alivyo na kuishi kama anavyotaka.
Aliondoka Orlando Pirates ya Afrika Kusini akiwa na kipaji maridhawa akaacha kesi ya gari la wizi ikimuandama. Akaenda zake Congo kucheza AS Vita kwa muda mfupi. Akarudi zake Ghana ambako Injinia Hersi Said alimfuata mpaka kijijini kwao kwa ajili ya kuja kucheza Yanga. Alionyesha kipaji maridhawa. Jina lilibadilika na kuwa BM33 kutokana na jezi aliyokuwa akivaa.
Baadaye wote tunajua kilichotokea akiwa Yanga. kesi yake ya CAS akalazimisha kuondoka Yanga kwenda kwa watani wao Simba, huku akiwa amejenga urafiki mkubwa na marehemu Zacharia Hans Poppe. Yanga waliachwa na maumivu makubwa kifuani.
Wasingeweza kusamehe wala kusahau. Kule alipewa jina jipya la BM3, kwani alikuwa akivaa jezi namba tatu iliyowahi kuvalia na Haruna Moshi ‘Boban’. Jina linabadilika. Alipoenda Simba, kama ilivyokuwa Yanga, alionyesha kipaji kikubwa lakini usumbufu ukawa mkubwa zaidi ya kipaji. Ni kama msichana mrembo aliyevaa sketi fupi. Kuna kitu unatamani kukiona zaidi kutoka kwake lakini haukioni🫠Unaishia katika matamanio tu. Ben alikuwa kama yule wa siku za mwisho wakati anakaribua kuondoka Yanga.