Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limetangaza rasmi kuahirisha michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ambayo ilikuwa imepangwa kuanza Februari 1, 2025, nchini Kenya, Tanzania, na Uganda.
Michuano hiyo sasa imepangwa kufanyika Agosti 2025.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya wataalam wa kiufundi na miundombinu kutoka CAF kulishauri shirikisho hilo kutoa muda zaidi kwa nchi waandaji ili kuboresha viwango vya miundombinu ya viwanja, mazoezi, hoteli na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya mashindano hayo makubwa.
Rais wa CAF, Patrice Motsepe amepongeza juhudi za marais wa nchi hizo tatu, William Ruto wa Kenya, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, na Yoweri Museveni wa Uganda kwa juhudi zao kubwa katika kuboresha miundombinu.
Hii ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo kufanyika kwa ushirikiano wa nchi hizo tatu.
Droo ya michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kesho, Januari 15, 2025, jijini Nairobi, Kenya, kuanzia saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.