Ilifikia wakati Barbara Gonzalez aliyekuwa CEO wa Simba aliamua kumfungia kwa utovu wa nidhamu. Yanga wakawacheka Simba. Wakawakejeli kwamba kunguru alikuwa hafugiki. Baadae Ben akafanya vituko akamaliza mkataba wake huku Yanga wakimsubiri kwa lengo ya kumrudisha mtoto nyumbani huku wakiwakejeli Simba.
.
Hatimaye akarudi Yanga. Akarudi nyumbani. Kama kawaida yake alionyesha dalili ya kipaji maridhawa lakini kipaji hicho kilizidiwa nguvu na vituko maridhawa. Kuna wakati alikwenda kwao Ghana akakaa miezi miwili wakati Ligi inaendelea. Safari hii ikawa zamu ya Simba kuwacheka Yanga. Waswahili wanasema ‘muosha huoshwa’ wakati wazungu wanasema ‘what goes around comes around’.😀
.
Alipomaliza mkataba wake Yanga hawakuwa na hamu naye. Na hapo hapo Simba hawakuwa na hamu naye. Na hapa ndipo Morrison alipozichanganya karata zake vibaya. Aliweza kuwafanya Yanga wajinga mara mbili lakini asingeweza kuwafanya Simba wajinga mara mbili. Angekuwa na akili angejua kwamba kurudi kwake Yanga kulikuwa kunamaanisha hiyo ilikuwa kete yake ya mwisho kwa hizi timu.
.
Simba walijua kwamba huo ndio ungekuwa mchezo wa Morrison. Unaharibu huku ukiwa na imani utarudi kule. Simba hawakutaka kufanywa wajinga mara mbili. Wakafunga milango.
.
Akakimbilia zake FAR Rabat ya Morocco. Nilijua asingetoboa. Hata kama asingepata majeraha lakini asingeta raha ya kuishi Morocco. Nimefika mara tatu pale Morocco. Napafahamu. Wana starehe zao lakini kwa mtu ambaye ulizoea starehe na sifa za jiji la Dar es Salaam kama ilivyokuwa kwa Morrison basi ingekuwa vigumu kwake kuishi Morocco.
.
Haishangazi kuona hata Clatous Chama na Tuisila Kisinda walipopata bahati ya kurudi tena Dar es Salaam kucheza Simba na Yanga hawakusita mara mbili. Dar ina utamu wake. Mtazame namna Aziz Ki anavyoishi. Asingeweza kuondoka kirahisi Dar es Salaam. Jiji ambalo linakufanya uwe mfalme kiurahisi tu
Edo Kumwembe