Mwanasiasa maarufu Godbless Lema amemshutumu mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kwa kufunga barabara kuu katikati ya jiji wakati wa sherehe za mwaka mpya.
Lema, ambaye ni mbunge wa zamani wa Arusha, amesema hatua hiyo ni ya kijinga na haina mantiki, kwani kuna maeneo mengine ya wazi ambayo yangeweza kutumika kwa mikusanyiko ya umma bila kuathiri miundombinu ya jiji.
Kupitia mtandao wa X, Lema alisema, "Nilikuwa safari nimerudi, nimeambiwa Mwaka mpya ulifunga barabara katikati ya mji. Huu ni ujinga na sifa za kitoto, kwani kuna maeneo mengi ya wazi ambayo yangeweza kutumika kwa public gathering bila kuathiri barabara na watumiaji."
Aliongeza kusema kuwa sasa amerejea na atakuwa na muda wa kufuatilia hatua za Makonda, na alionya kwamba viongozi wa aina hiyo wanapaswa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Lema pia alikosoa hatua hiyo kwa kusema kuwa ilileta usumbufu kwa wakazi wa jiji, na kutoa wito kwa viongozi wa serikali kutafuta mbinu bora za kufanya mikusanyiko ya umma bila kuingilia shughuli za kila siku za watu.