Katika event ya uapisho wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Rais wa zamani, Barack Obama alionekana akiingia akiwa peke yake bila mkewe, Michelle Obama.
Jambo hilo ni kinyume na desturi za Wamarekani ambapo huwa imezoeleka kwamba marais wastaafu lazima waongozane na wake zao kwenye shughuli za kitaifa, likiwemo tukio kubwa kama la kuapishwa kwa Trump.
Tukio hilo linakuja siku chache baada ya Michelle kutoonekana tena akiwa na mumewe kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa Marekani, Jimmy Carter.
Mengi yanazungumzwa kuhusu kutoonekana kwa Michelle akiwa na mumewe, wapo wanaoeleza kuwa anasimamia msimamo wake wa kuonesha hadharani kutomuunga mkono Trump lakini wengine wanaenda mbali zaidi na kudai kuwa wawili hao hawapo sawa na ndoa yao ipo mashakani.
Japo Michelle hakuwa ametoa sababu yoyote ya kutoshiriki kwenye uapisho huo, vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa ameamua kukaa mbali kwa sababu hamuungi mkono Trump na si vinginevyo.
Wakati wa kampeni zilizomuingiza madarakani Trump, Obama na mkewe walikuwa wakimpigia kampeni Kamala Harris ambaye hata hivyo kura hazikutosha lakini siku chache baadaye, Trump na Obama walionekana wakiwa wamekaa pamoja kwenye mazishi ya Carter, jambo ambalo pia liliibua gumzo kubwa.
Wakati wa uapisho hapo jana, wafuasi wa Trump walisikika wakipiga kelele wakati Obama akiingia akiwa peke yake bila mkewe.
Je, kukosekana kwa Michelle kwenye uapisho huo ni kwa sababu ya kutomuunga mkono Trump au kuna shida kwenye ndoa yao? Tuache muda uzungumze.