KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, anajiandaa kukamilisha hesabu za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kikubwa huku Wekundu wa Msimbazi wakielekea Angola kwa mchezo mwingine mgumu dhidi ya Bravos do Maquis, utakaochezwa Jumapili hii Januari 12, 2025. Fadlu anajua wazi kwamba mchezo huo utakuwa na changamoto kwao lakini amesema: “Tutafuzu kikubwa.”
Fadlu ameona kuna matumaini ya kwenda robo fainali baada ya kufanya vizuri katika mchezo uliopita huko Tunisia.
Simba iliwapa furaha kubwa mashabiki wake wikiendi iliyopita, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya CS Sfaxien kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, Tunisia. Ushindi huo umewafanya wafikishe pointi tisa, sawa na CS Constantine, ambao wanashika nafasi ya kwanza kwenye kundi A.
Huu ni ushindi muhimu ambao unaifanya Simba kuwa na nafasi nzuri ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali, lakini bado kuna kazi kubwa mbele yao.
Kocha Fadlu Davids alionyesha furaha yake na kusema: “Kwanza kabisa, napenda kutoa pongezi kwa wachezaji wangu. Walifanya kazi nzuri, walimudu mpango wetu wa mchezo na kuufanyia kazi vizuri uwanjani. Haikuwa rahisi, lakini tumefanikisha kile ambacho tulikuwa tukikihitaji. Hata hivyo, bado tuna kazi kubwa ya kufanya, hatuwezi kupumzika.”
Fadlu anajua kuwa mchezo ujao dhidi ya Bravos do Maquis utakuwa na changamoto tofauti na ule wa awali, ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 la penalti ya Jean Charles Ahoua dhidi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha huyo anatarajia mchezo wa Angola utakuwa mgumu zaidi kutokana na mazingira ya uwanja na upinzani, ambao wanahitaji kushinda ili kubaki na matumaini ya kufuzu.
“Katika mchezo wa kwanza, tulifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0, lakini huko Angola hali itakuwa tofauti. Tutakutana na timu ambayo itakuwa na morali ya kutaka kuweka sawa mambo baada ya kupoteza ugenini kwenye mchezo wao uliopita, hivyo ni lazima tuwe makini na kuelewa changamoto tutakazokutana nazo,” aliongeza Fadlu.
Kwa upande wake, nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alizungumzia hali ya Bravos do Maquis, akikiri kwamba timu hiyo itakuwa na presha kubwa baada ya kipigo kizito cha mabao 4-0 walichopata kutoka kwa CS Constantine.
“Tunajua watakuja kwa nguvu ili kujitahidi kurekebisha makosa yao lakini hii ni Simba hivyo tutapambana kufanikisha malengo yetu,” alisema Tshabalala.
Kocha Mario Soares wa Bravos alikiri kwamba timu yake inahitaji kurekebisha makosa ya mchezo uliopita kabla ya kukabiliana na Simba.
“Tunahitaji kujitoa kwa nguvu, kuonyesha kwamba bado tunaweza kushindana. Kipigo cha Constantine kimeonekana kuwa kichungu, lakini tunataka kutengeneza njia ya kufufuka mbele ya mashabiki wetu,” alisema Soares.
Simba, ikiwa na pointi tisa, iko katika nafasi nzuri ya kufuzu, lakini mchezo wa Angola utakuwa na maana kubwa, kwani utakuwa na uamuzi wa kufuzu moja kwa moja au kusubiri mchezo wa mwisho ambao watakuwa nyumbani dhidi ya Constantine.
Kwa Bravos do Maquis, hii ni mechi ya lazima kushinda, kwani kipigo kingine kitawatibulia. Mchezo huo utakuwa na mvuto mkubwa, na mashabiki wa soka wataendelea kuwa na shauku ya kuona ni nani atabaki na nafasi ya kuendelea kupigania taji la Kombe la Shirikisho Afrika.
UGUMU UKO HAPA
Hata hivyo, wakati hesabu za Fadlu zikiwa hivyo kuna hatari ya kundi hilo kushangaza wengi siku ya mwisho Januari 19, kwani kuna timu inaweza kuwa na pointi 12 na isiende robo fainali.
Mshangao huo unaweza kutokea kama timu zote tatu kwa maana ya CS Constantine, Simba na Bravos zikifikisha pointi 12 huku zikitakiwa mbili kwenda robo fainali na moja kubaki. Hiyo inaweza kutokea endapo Bravos ikishinda mechi mbili zilizobaki dhidi ya Simba na CS Sfaxien. Lakini pia Simba ikiichapa CS Constantine mchezo wa mwisho nyumbani, huku CS Constantine wakishinda mchezo ujao dhidi ya CS Sfaxien wanaoonekana kuwa wanyonge wa kundi.
Ikitokea hivyo ambapo timu tatu zitakuwa na pointi 12 huku CS Sfaxien ikibaki haina kitu, itaangaliwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kuamua timu mbili za kwenda robo fainali.
Kanuni za mashindano hayo zinabainisha kwamba, endapo timu mbili zikilingana pointi kitu cha kwanza cha kuangalia ni matokeo ya wenyewe walipokutana yalikuwaje, lakini zikiwa timu tatu, suala la tofauti ya mabao ya kufunga na kufunga litachukua nafasi.
Kwa sasa ukichukua kanuni hiyo ya tofauti ya mabao, Constantine imefunga 9 na kuruhusu manne, ikiwa na tofauti ya mabao matano. Simba iliyofunga matano na kuruhusu matatu, tofauti yake ni mawili wakati Bravos imefunga sita na kufungwa tisa, ina deni la mabao matatu.