Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Mohamed Janabi, ameweka wazi umuhimu wa kuzingatia mtindo bora wa maisha kama kinga dhidi ya saratani.
Akizungumza kuhusu namna ya kupambana na ugonjwa huo, Dkt. Janabi ameeleza kwamba kila binadamu ana chembechembe za saratani mwilini, lakini kinga ya mwili inapambana kila siku ili kuzuia chembe hizo kugeuka ugonjwa.
Dkt. Janabi amesisitiza kuwa ushindi wa kinga ya mwili dhidi ya saratani unategemea zaidi mtindo wa maisha wa mtu. Amebainisha mambo kadhaa yanayoweza kusaidia kuimarisha kinga ya mwili, ikiwa ni pamoja na kupata usingizi wa kutosha, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kuongeza ulaji wa mboga za majani kwenye mlo wa kila siku, na kupunguza msongo wa mawazo (stress)
Ameeleza kuwa msongo wa mawazo ni moja ya vichocheo vikuu vya kuathiri kinga ya mwili. Stress husababisha kuongezeka kwa kichocheo kiitwacho cortisol, ambacho huongeza kiwango cha sukari mwilini na kudhoofisha kinga.
Akizungumzia aina za msongo wa mawazo, Dkt. Janabi ametaja msongo wa kijamii (social stress) kama changamoto kubwa. Ametoa mfano wa matatizo ya ndoa na familia, ambapo ugomvi wa mara kwa mara huchangia kuongezeka kwa kiwango cha cortisol mwilini.