Mchambuzi nguli wa soka wa Sky Sports, Paul Merson amemuonya Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim kwamba atahitaji kubadilisha mbinu zake ili kufanikiwa akiwa na Manchester United.
Merson amesema kuwa Amorim lazima atambue kuwa Ligi Kuu ya Uingereza ipo kwenye kiwango tofauti kabisa na soka la Ureno, huku Manchester United wakijiandaa kukabiliana na Liverpool kwenye mchezo wa Super Sunday.
Kocha huyo, ambaye alichukua nafasi ya Erik ten Hag Novemba, 2024 baada ya kujiunga kutoka Sporting Lisbon ya Ureno, amekuwa na changamoto za kupata matokeo na kuonyesha uwezo tangu alipowasili Old Trafford.
Baada ya ushindi dhidi ya Manchester City kwa mabao 2-1, Manchester United wamepoteza mechi nne mfululizo katika mashindano yote, ikiwa ni pamoja na kipigo cha 2-0 dhidi ya Newcastle.
Hali hii ilimfanya Amorim akiri kwamba timu yake iko kwenye vita ya kuepuka kushuka daraja.
Mambo hayatakuwa rahisi kwani wanakutana na Liverpool yenye kiwango bora na inayoongoza Ligi Kuu tena kwenye Dimba la Anfield.
Akizungumza kwenye kipindi cha The Football Show, Merson alielezea maoni yake kuhusu hali ya sasa ya Manchester United na kwa nini Amorim anahitaji kubadilika haraka ili kuhimili changamoto za Ligi Kuu ya Uingereza.
"Kwa fomu yao ya sasa, huenda kocha yuko sahihi kusema wako kwenye vita ya kushuka daraja. Wanacheza na Southampton nyumbani katika mechi yao ijayo ya ligi, na ingawa ungetarajia washinde mechi hiyo, kwa sasa si jambo la kufurahisha kuangalia," alisema Merson.