Kocha wa Simba SC, Fadlu Davids ameweka wazi timu yake inajivunia kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini amesisitiza bado wanakusudia kufanya jambo wakiwa Kwa Mkapa.
.
Mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, Simba iliotoka sare ya 1-1, uliwafanya vijana hao wa Fadlu kutinga hatua hiyo baada ya kufikisha pointi 10 katika kundi A nyuma ya CS Constantine wenye pointi 12 huku ikiwa imesalia raundi moja kutamatisha hatua ya makundi na itacheza wikiendi hii nyumbani dhidi ya CS Constantine.
.
“Tulikuwa na malengo ya kufuzu mapema na sasa tumefanikiwa. Lakini bado kuna jambo moja muhimu na hilo ni kumaliza kileleni mwa kundi letu,” alisema kocha Fadlu na kuongeza.
.
“Mchezo dhidi ya CS Constantine ni muhimu sana kwetu, ni mchezo wa kutafuta pointi tatu zitakazokaa na kutufikisha kwenye kilele cha kundi. Itakuwa mechi ngumu kwa sababu CS Constantine ni timu nzuri na wanajua kucheza mechi kubwa,”
.
“Tutahitaji kuwa makini na kujitahidi kuvunja ulinzi wao, lakini tuna uwezo wa kushinda kama tutakuwa na mchezo wetu wa kushambulia na kumiliki mpira.”