Kwa Mipango Hii ya Yanga, Waarabu Hawana Chao Leo.....

 

Kwa Mipango Hii ya Yanga, Waarabu Hawana Chao Leo.....

YANGA imekamilisha kazi ya kwanza ugenini kwa kuichapa Al Hila bao 1-0 juzi Jumapili, kazi ya pili iliyobaki ni kuichapa MC Alger Jumamosi ya wiki hii pale Benjamin Mkapa, kisha kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa Yanga, Sead Ramovic ameuona ugumu uliopo mbele yake kuikabili MC Alger, hivyo ametaja mambo ambayo yatafanikisha jambo hilo na kuwapa furaha Wananchi.

Yanga itakutana na MC Alger Jumamosi Januari 18 kwenye mchezo wa mwisho wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao kati ya timu hizo mbili moja itaungana na Al Hilal ya Sudan kwenda robo fainali.

Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa utaamua hatma ya klabu hizo mbili ambapo Yanga yenye pointi saba ikiwa kwenye nafasi ya tatu itahitaji ushindi ili ifuzu huku MC Alger yenye pointi nane itahitaji japo sare tu ili kushika nafasi ya pili inayowaniwa na timu zote mbili.

Ramovic alisema katika kufanikisha malengo yao, kwanza amewazuia wachezaji wake kushangilia kupitiliza ushindi dhidi ya Al Hilal akisema anataka kuona kila akili ya mchezaji wake inajipanga kwa ajili ya mchezo ujao.

Ramovic alisema amefurahishwa na namna wachezaji wake walivyojituma kwenye mechi zao tatu za mwisho akiona morali ikiendelea kupanda na sasa wana mlima kwenye mechi ya mwisho ambayo kwao ni kama fainali.

Kocha huyo Mjerumani ambaye anaendelea kuibadilisha timu hiyo kwa kasi, alisema anajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini ana imani na namna wachezaji wake wanavyoonyesha njaa ya kutafuta ushindi.

“Hii mechi (dhidi ya Al Hilal) imekwisha, niliwaambia wachezaji baada ya kutoka ndani ya uwanja kila mmoja asitishe furaha yake, tunatakiwa kujiona kama hatujafanya kitu na tukitakiwa kwenda kufanya kitu kikubwa zaidi kwenye mchezo ujao wa nyumbani,” alisema Ramovic na kuongeza:

“Tunatakiwa kushinda mechi ya mwisho kwa nguvu licha ya kwamba haitakuwa rahisi, MC Alger nao wanapitia mabadiliko kwenye timu yao tofauti na walivyoanza mechi za makundi, tunachotakiwa ni kuongeza umakini kwenye mechi hii ya mwisho.

“Tutakuwa nyumbani na wao walishinda dhidi yetu wakiwa kwao, tumekuwa na mabadiliko mazuri ndani ya timu yetu tofauti na mechi mbili za kwanza tulizocheza na tumeanza kuimarika kwa nguvu, nawapo-ngeza sana wachezaji wangu, lakini wanatakiwa kutambua tunakwenda kucheza mechi ngumu itakayobeba heshima yetu.”

Aidha, Ramovic amekiri kwamba timu yake ilistahili kushinda kwa mabao mengi dhidi ya Al Hilal ambayo ilipoteza mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya Yanga akisema wanakwenda kuwaongezea utulivu wa wachezaji wao ili watumie nafasi wanazotengeneza.

“Ni kweli tungeweza kupata mabao zaidi, tulitengeneza nafasi nyingi lakini ile ni mechi ambayo tulitakiwa kushinda tena dhidi ya timu iliyocheza kwa ubora mechi zake nne za kwanza, kulikuwa na ugumu na presha ilikuwa kubwa.

“Tutazungumza na wachezaji kuwaongezea utulivu ili makosa ya kupoteza nafasi yasiendelee, tukicheza kwa umakini zaidi ya ule tuliouonyesha dhidi ya TP Mazembe tunaweza kufanikiwa kirahisi.”

Yanga inasaka kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kufanya hivyo ikiwa chini ya kocha Miguel Gamondi ambapo iliishia hatua hiyo ikifungwa kwa penalti 3-2 dhidi ya Mamelodi Sundowns baada ya nyumbani na ugenini kutoka 0-0.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad