WAKATI KenGold ikiendelea kuimarisha kikosi, macho na masikio ya wadau na mashabiki wa timu hiyo jijini Mbeya ni kuona staa kutoka Ghana, Bernard Morison akitua kwa wachimbaji hao wa madini.
KenGold inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, haijawa na matokeo mazuri ikiwa mkiani kwa pointi sita ambapo matumaini yao ni kuona wanapambana kutoshuka daraja.
Hadi sasa timu hiyo tayari imeongeza nyota wapya watano wakiwa ni Sadala Lipangile, Mathias Juviliani (KVZ), Abdalah Nassir (Miembeni), Sambale Komanji (Tabora United) na Steven Dua.
Tetesi zilizosambaa ni kuwa wachimbaji hao wa dhahabu ni kuwa wanamuwinda staa wa zamani wa Yanga na Simba, Morrison ambaye kwa sasa yupo hapa nchini akiwa hana timu na muda wowote huenda akavaa uzi wa timu hiyo.
Katibu Mkuu wa KenGold, Benson Mkocha, alisema ni mapema kuthibitisha taarifa hizo kwa kuwa bado hawajamalizana naye, hivyo kukubali haraka lolote linaweza kutokea kwani Morrison ni mchezaji mwenye jina kubwa.
Alisema baada ya kukamilisha mazungumzo na kukubaliana naye uongozi utaweka wazi, huku akieleza kuwa mzunguko wa pili wanahitaji kurejesha hadhi na heshima ya timu.
“Nadhani tusubiri kwanza hizo taarifa, tukikubaliana naye tutaweka wazi, kimsingi tunaendelea kusuka timu na tayari tumesainisha watano, tukilenga mzunguko wa pili tufanye vizuri” alisema Mkocha.
Kigogo huyo aliongeza kuwa wanafahamu ugumu walionao, akisisitiza kuwa wanaoitabiria timu hiyo kushuka daraja wawe na akiba ya maneno kwani mpira unayo maajabu yake.