Wachunguzi wa ajali ya Ndege ya Jeju Air aina ya Boeing 737-800, iliyotokea mwezi uliopita Korea Kusini na kusababisha vifo vya Watu 179, wamebaini uwepo wa manyoya na damu za ndege (wanyama) kwenye injini zote mbili ambapo Ndege hiyo ilikuwa ikitoka Bangkok, Thailand kuelekea Muan, Korea Kusini, kabla ya kutoka nje ya njia ya kurukia na kulipuka baada ya kugonga kingo za Uwanja wa Ndege.
Dakika chache kabla ya ajali, Rubani aliripoti kugongwa na ndege (bird strike) kwenye injini na kutangaza hali ya dharura akijaribu kutua kwa mzunguko upande mwingine wa Uwanja na licha ya tahadhari iliyotolewa na mamlaka za anga kuhusu uwepo wa ndege (wanyama) eneo hilo, ajali hiyo haikuweza kuepukika.
Aidha Wachunguzi wa qjali wamesema black box ya ndege hiyo (Kifaa maalumu cha kurekodi data) iliacha kurekodi data dakika nne kabla ya ajali, hali inayozua maswali kuhusu uwezekano wa kukatika kwa mifumo yote ya umeme, jambo ambalo ni nadra sana kutokea.
Sim Jai-dong, Mtaalamu wa uchunguzi wa ajali za anga, amesema kuwa matukio ya Ndege kugongwa na Ndege (wanyama) kwenye injini zote mbili ni nadra ingawa historia imeonyesha kuwa ajali kama hizo zinaweza kumalizika bila vifo kama ilivyotokea kwenye tukio la “Miracle on the Hudson” mwaka 2009 Nchini Marekani , uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo kamili cha ajali hii mbaya zaidi katika historia ya anga ya Korea Kusini.